Rais Biden aanza ziara ya siku mbili nchini Angola
2 Desemba 2024Rais wa Marekani Joe Biden amesafiri kuelekea nchini Angola atakapoanza siku ya Jumatatu ziara yake ya siku mbili yenye lengo la kukabiliana ushawishi wa China na pia kutimiza ahadi muhimu aliyoitowa mwaka 2022 ya kuimarisha mahusiano na bara la Afrika.
Kabla ya kuelekea Angola, Biden alitarajiwa kutua kwa muda mfupi katika taifa la Afrika Magharibi la Cape Verde mapema leo asubuhi, na kukutana na Waziri Mkuu Ulisses Correia e Silva.
Biden atakuwa na mkutano na rais Joao Lourenco wa Angola na atatembelea makumbusho ya Kitaifa ya Utumwa katika mji mkuu Luanda. Ziara ya Biden itajikita zaidi kwenye mradi mkubwa wa reli unaounganisha bandari ya Lobito ya Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia zenye utajiri wa rasilimali.
Rekodi zinaonesha kuwa Biden ni rais wa kwanza wa Marekani kuitembelea nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika yenye utajiri wa mafuta, tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Wareno mwaka 1975.