1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Haiti walalamikia ukosefu wa msaada

18 Agosti 2021

Raia wa Haiti walioachwa bila makazi kufuatia tetemeko kubwa la ardhi wameelezea hasira zao kuhusiana na ukosefu wa msaada kutoka kwa serikali huku wakilala nje kwa siku ya nne mfululizo.

https://p.dw.com/p/3z7Ce
Haiti | Erdbeben
Picha: Joseph Odelyn/AP/dpa/picture alliance

Waziri mkuu Ariel Henry, aliyezuru mji ulioathirika zaidi wa Les Cayes Kusini Magharibi mwa Haiti muda tu baada ya tetemeko hilo la  ardhi la Jumamosi lililokuwa na ukubwa wa 7.2 katika kipimo cha richter alipongeza utulivu ulioneshwa na manusura wa tetemeko hilo na kuahidi msaada wa haraka.

Lakini kufikia jana jioni wakati mawingu yakitandaa tena kwa siku ya pili ya mvua kubwa, wakazi katika mji huo uliojaa mahema, walisema kuwa msaada ni wa kiwango cha chini mno. Roosevelt Milford, kasisi aliyetembelea vituo vya redio na televisheni katika eneo hilo akiomba fursa ya kusikika, alisema kuwa hakuna mtu yeyote kutoka kwa serikali aliyefika katika eneo hilo na kwamba hakuna lolote lililofanyika kufikia sasa. Akizungumza kwa niaba ya wakazi wote waliopiga kambi katika mahema yaliojengwa katika ardhi iliyojaa matope, Milford alisema kuwa wanahitaji msaada.

Haiti I  Ariel Henry wird Premierminister
Ariel Henry - Waziri mkuu wa HaitiPicha: Matias Delacroix/AP/picture alliance

Wasiwasi wa usalama katika maeneo yanayodhibitiwa na magenge katika barabara kutoka mji mkuu wa Port -au-Prince pamoja na barabara zilizoharibiwa na tetemeko hilo, umefanya kuwa vigumu kwa makundi ya msaada na uokoaji kufikia baadhi ya sehemu zilizoathirika zaidi. Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema jana kuwa mazungumzo yaliopata ufanisi na makundi yaliojihamii yaliruhusu msafara wa makundi ya kutoa msaada wa kibinadamu kufika Les Cayes. Vyombo vya habari vimeripoti kuwa makubaliano yameafikiwa na magenge hayo.

Jerry Chandler, mkuu wa shirika la ulinzi wa raia nchini Haiti linaloshughulikia msaada wa dharura, amesema kuwa serikali ilikuwa inatuma msaada katika maeneo yalioathirika kwa kutumia barabara na kwamba katika siku za kwanza za tetemeko hilo la ardhi, madaktari wengi na wafanyakazi wa mashirika ya msaada walifika kwa haraka katika maeneo hayo kwa kutumia ndege. Lakini mafuriko na maporomoko ya ardhi baada ya kimbunga Grace ambacho kilipita Jamaica kufikia jana alasiri, vimefanya kuwa vigumu zaidi kufikia maeneo ya mashammbani.