1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Afrika Kusini washiriki uchaguzi Mkuu

29 Mei 2024

Raia wa Afrika Kusini wanapiga kura katika uchaguzi wa saba tangu ilipoingia katika utawala wa kidemokrasia. Chama tawala ANC kinahitaji kupata asilimia 50 au zaidi ili pasiwepo na serikali ya mseto.

https://p.dw.com/p/4gQPt
Uchaguzi Afrika Kusini 2024
Raia wa Afrika Kusini wanapiga kura baada ya miaka 30 tangu taifa hilo lipate uhuru. Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Chama cha ANC ambacho kinaongozwa na Rais Cyril Ramaphosa kinakabiliwa na shinikizo kubwa. Rais Ramaphosa ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho kitaifa, alipiga kura katika eneo alilokulia la Chiawelo lililopo kitongoji maarufu cha Soweto, jijini Johannesburg, amesema amefurahishwa na namna zoezi la upigaji kura linavyokwenda.

Rais wa zamani na kiongozi wa Chama cha MK, Jacob Zuma, naye alipiga kura yake katika Shule ya Msingi ya Ntolwane huko Nkandla majira ya alasiri huku Julius Malema kiongozi wa chama cha EFF alipiga kura katika jimbo alilozaliwa la Limpompo kaskazini mwa taifa hilo.


Waangalizi wanaofuatilia zoezi hili pia wamesema hawajaona hitilafu zozote kama alivyoniambia Pumelele Mokele muangalizi kutoka chuo kikuu cha Afrika Kusini, UNISA. Naye Profesa Daniel Lomberd na mke wake asubuhi na mapema hii leo walifika katika kituo cha kupigia kura cha union Buliding, kilichopo ndani ya bustani ya ikulu ya Afrika Kusini. Ameniambia amepiga kura yake salama na kwamba anategemea mabadiliko.
 
Uchaguzi unafanyika wakati taifa likikumbwa na changamoto chungu nzima

Uchaguzi Afrika Kusini 2024
Waafrika Kusini washiriki uchaguzi Mkuu Picha: PHILL MAGAKOE/AFP

Waafrika Kusini wanapiga kura huku taifa lao likikumbwa na changamoto nyingi, ikiwemo tatizo la umeme, maji, rushwa, uhalifu na tatizo la watu weusi kukosa ardhi iliyonyakuliwa na wazungu.

Ni kwa sababu hiyo Simon Thintole kijana aliyehitimu chuo kikuu mwaka huu, na mwenye matumaini ya kuajiriwa amepiga kura kwa matumaini ya kupatikana mabadiliko. Mpaka sasa watu wanaendelea kupiga kura na hali ni shwari hakuna taarifa zozote za uvunjifu wa usalama. Vituo vya kupigia kura vinatarajiwa kufungwa mwendo wa saa tatu usiku na kupisha zoezi la kuhesabu kura litakaloendelea sambamba na kutangazwa matokeo ya awali.