1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasema maandamano hayatakoma hadi raia wachukue usukani

Faiz Musa26 Aprili 2019

Maelfu ya raia wanaondamana nchini Sudan kutoka kila pembe ya nchi hiyo wamejazana katika makao makuu ya jeshi wakishinikiza kuondolewa kwa uongozi wa jeshi na kutaka uongozi wa kiraia.

https://p.dw.com/p/3HUMW
Sudan Demonstration in Khartum
Picha: picture-alliance/AA/M. Hjaj

Muungano huo wa Wasomi wa Sudan, SPA, ambao uliongoza maandamano ya miezi kadhaa yaliyosababisha kuondolewa madarakani kwa Omar Al Bashir umesema maandamano yao ya mapinduzi hayatakoma hadi pale raia watakapochukua usukani wa taifa hilo.

Wakizungumza na wanahabari viongozi wa SPA walisema kwamba hadi pale jeshi litakapokabidhi uongozi wa serikali hiyo ya mpito kwa raia na mahitaji yao yote kutimizwa ndipo watakapoacha kuingia barabarani.

Msemaji wa baraza la jeshi la Sudan, Shams Al-Deen Al-Kabashi alisema kwamba wananuia kuendelea kuongoza serikali ya mpito na kudumisha uhuru wa taifa hilo huku baraza la mawaziri likiwa mikononi mwa raia, kauli ambayo inatarajiwa kuongeza hasira za waandamanji ambao wanataka jeshi kuachia madaraka mara moja kwa raia na uwakilishi wa jeshi uwe mchache katika serikali ya mpito.

Sudan Demonstration in Khartum
Wasudan wakiwa katika maandamano nje ya makao makuu ya jeshiPicha: picture-alliance/AA/M. Hjaj

Wakiwa wamejazana mjini humo na kukaa nje ya makao makuu ya jeshi waandamanaji hao wamebeba mabango, wanapiga ngoma na kuimba nyimbo za mapinduzi.

Raia wasema wana imani matakwa yao kutimizwa.

Mmoja wa waandamanji hao Merghani Hussein amesema wana imani raia watapata uongozi.

"Tuna imani jeshi litatupa uongozi wa serikali ya mpito na mkuu wa baraza la jeshi la mpito amesema atafanya hivyo wakikubaliana. Mahitaji yetu yote yamepitiwa kwa makini, yanajulikana na tunashinikiza yatimizwe jinsi yalivyo. Hatutaondoka hapa hadi matakwa yetu yote yatakapotimizwa, ambapo moja wapo ni kutaka serikali ya raia," alisema Hussein.

Siku ya Alhamisi mwanaharakati Ahmed Najdi alisema wanatarajia baraza la serikali ya mpito linalojumuisha jeshi na raia ambalo huenda ikawa ni hatua ya kati kwa kati ambayo wengi wa waandamanaji wataikubali, ila kabla ya hilo kuafikiwa wanaendelea na maandamano ya usiku na mchana.

Tangu kupata uhuru wake taifa la Sudan lina historia ya uongozi mrefu wa kidikteta wa kijeshi ambapo baadhi ya wananchi sasa wanasema hawana imani na vyama va kisiasa kwa sababu vimekuwa vikishirikiana na uongozi huo wa kidekteta ili kuweza kupata viti vingi vya ubunge ama nafasi za wizara.

Mohammed Al-Neel kijana mwenye umri wa miaka 25 anasema muungano wa wasomi wa Sudan, SPA, unaungwa mkono na raia kwa sababu wao hawakuegemea upande wowote.

 

(AFPE/APE)