1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar 2022: Argentina, Poland na Australia zatinga 16 bora

Daniel Gakuba
30 Novemba 2022

Argentina ya Lionel Messi imesonga mbele katika duru ya mtoano baada ya kuishinda Poland magoli 2-0 na kuonyesha mchezo wa kiwango cha juu kabisa. Poland na Australia pia zavuka salama ngazi ya makundi.

https://p.dw.com/p/4KJit
Poland v Argentina: Group C - FIFA World Cup Qatar 2022
Picha: Clive Brunskill/Getty Images

Katika kundi C Argentina ambayo tangu dakika ya kwanza ya mchezo ilionekana kuwa timu bora ilipata penelti mnamo dakika ya 39 baada ya nahodha wake, Messi kufanyiwa madhambi langoni, lakini Messi huyo huyo alishuhudia mkwaju wake ukipanguliwa na mlinda mlango wa Poland Wojciech Szczesny. 

Soma zaidi: Watetezi wa taji la kombe la Dunia, Ufaransa wailaza Australia mabao 4-1 huku Tunisia na Denmark zikitoka bila bila

Jeuri ya Poland iliyeyuka dakika ya kwanza ya kipindi cha pili kwa goli murua la Argentina lililofungwa na Alexis MacAllister, na dakika 10 baadaye Beki wa kushoto Marcos Acuna aliiweka Argentina katika nafasi salama zaidi kwa kuingiza kimiani bao la pili.

Ingawa hadi dakika ya mwisho ya mechi hiyo ya kuvutia Poland ilikuwa ikiendelea kufukuza vivuli vya wachezaji wa Argentina, timu hiyo ya Ulaya imemaliza katika nafasi ya pili na hivyo kuambatana wa washindi wao katika duru inayofuata.

FIFA World Cup Qatar 2022 - Group C - Saudi Arabia v Mexico
Ingawa Saudi Arabia na Mexico zimetolewa zimeonyesha mchezo safi kabisaPicha: MOLLY DARLINGTON/REUTERS

Mbio za Saudia na Mexico zaishia ukingoni

Mechi nyingine katika kundi hilo la C ilikuwa kati ya Saudi Arabia na Mexico, na ilimalizika kwa ushindi wa Mexico wa magoli 2-1.

Mexico ambayo ilimaliza pia na pointi nne sawa na Poland ilihitaji goli moja tu la ziada ili uamuzi juu ya timu itakayoendelea ufikiwe kwa msingi wa nidhamu, ilikatishwa tamaa pale Saudi Arabia waliocheza sehemu kubwa ya mchezo wakilazwa 2-0 walipofunga bao lao katika dakika za nyongeza.

Soma zaidi: Kombe la Dunia 2022: Senegal imekuwa nchi ya kwanza ya Afrika kuvuka ngazi ya makundi

Katika kundi D timu pekee kutoka Afrika iliyocheza jana, Tunisia ilipata ushindi wa kihistoria dhidi ya mkoloni wake wa zamani, Ufaransa, lakini ushindi huo wa goli 1-0 haukuisaidia chochote kwani imemaliza katika nafasi ya tatu na kuyaaga mashindano.

Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps ambaye timu yake ilikuwa tayari imefuzu kwa awamu ya 16 za mwisho aliwapumzisha wachezaji wake karibu wote walioanza uwanjani katika mechi mbili za awali, na kuwapa nafasi wale ambao walikuwa wakilichemsha benki kama wachezaji wa akiba.

FIFA World Cup Qatar | Frankreich gegen Tunesien
Katika mechi yake ya tatu, kocha wa Ufaransa aliwapumzisha wachezaji vigogoPicha: SIPHIWE SIBEKO/REUTERS

Fursa kwa wachemsha benchi

Deschamps amepuuza waliomkosoa kwa hoja kuwa ameshindwa mechi ya tatu kwa kuidharau Tunisia, akisema alitaka wachezaji walioshinda mechi mbili za awali wakusanye nguvu za kutosha, kwa sababu mechi nyingi katika mashindano haya hudumu kwa dakika 100 badala ya 90 zilizozoweleka.

Kocha wa Tunisia amesema licha ya kufunga virago mashabiki wa timu yake wanayo ya kujivunia, yakiwemo kukutoka sare na Denmark na kuwashinda mabingwa wa dunia, Ufaransa.

Soma zaidi: Kombe la Dunia: Brazil na Ureno zafuzu duru ya mtoano

Mbali na Ufaransa timu nyingine iliyonusurika ni Australia iliyoishinda Denmark goli 1-0, na kutimiza pointi sita sawa na Ufaransa lakini ikiwa na idadi ndogo ya magoli.

Baada ya hapa, Argentina watakutana na Australia, huku Poland ikiweka miadi na mabingwa wa dunia Ufaransa katika mechi za kuania nafasi ya kucheza robo fainali

Vyanzo: afpe, rtre