1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin na Erdogan waijadili Idlib

17 Septemba 2018

Rais wa Urusi Vladimir Putin amekutana na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyipp Erdogan hii leo kujaribu kuafikiana juu ya mustakabali wa jimbo la Idlib linalodhibitiwa na waasi nchini Syria.

https://p.dw.com/p/351O6
Iran Teheran Syrien Gipfel - Putin trifft Erdogan
Picha: Reuters/Turkish Presidential Palace/C. Oksuz

Rais wa Urusi Vladimir Putin amekutana na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyipp Erdogan hii leo kujaribu kuafikiana juu ya mustakabali wa jimbo la Idlib linalodhibitiwa na waasi nchini Syria. Wakuu hao wawili, wana misimamo inayotofautiana lakini wanaosalia kuwa washirika wakuu wa kimataifa katika mzozo huo wa Syria, uliodumu kwa miaka saba sasa. 

Mwanzoni tu mwa mazungumzo yao, Rais Vladimir Putin ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo alisema ulikuwa muhimu sana. Alinukuliwa akisema, "Kuna masuala mengi ya kujadili na miongoni mwake ni masuala magumu." Na kwa upande wake rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan alisema "Nadhani sio tu kikanda, lakini dunia nzima inautupia jicho mkutano wetu wa leo. Naamini taarifa tutakayoitoa baada ya mkutano wa Sochi itaashiria mwanzo mpya kwenye ukanda wetu.

Uturuki imekuwa ikijitahidi kuzuia mashambulizi makubwa yanayotarajiwa kufanywa kwenye jimbo hilo lililoko karibu na Uturuki, wakati vikosi vya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi, vikifanya maandalizi ya mashambulizi.

Umoja wa Mataifa na taasisi zisizo za kiserikali mara kwa mara zimeonya kwamba mashambulizi hayo huenda yakasababisha umwagaji damu mkubwa na janga la kibinaadamu katika jimbo hilo linalokaliwa na raia wanaokadiriwa kufikia milioni 3.

Syrien Angriffe Provinz Idlib
Moja ya eneo lililoshambuliwa kusini mwa jimbo la Idlib.Picha: Getty Images/AFP/A. Al-Dyab

Rais Putin ndiye mwenyeji wa mazunguzmo ya sasa.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin alikuwa mwenyeji wa mazungumzo kati yake na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, mjini Sochi. Wakuu hao wamekutana kwa lengo la kujadili juhudi za amani katika jimbo la Idlib, ambalo ni ngome ya mwisho ya waasi nchini Syria, linalokabiliwa na kitisho cha mashambulizi makubwa kutoka vikosi vya serikali.

Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov aliliambia shirika la habari la serikali la RIA kabla ya mazungumzo hayo kwamba, "hali ni tete" katika eneo hilo, hivyo Urusi inataka kile ilichokiita "mazungumzo makini na yatakayohusisha ngazi za juu zaidi".

Erdogan na Putin walikutana awali Septemba 7 mjini Tehran, walipofanya mkutano wa kilele wa siku tatu pamoja na rais Hassan Rouhani wa Iran, ambapo kulishudiwa kukinzana kwa wazi kati ya rais  Putin na Erdogan, kuhusu namna ya kuukabili mzozo wa eneo hilo, linalopakana na Uturuki.

Mkutano huu wa Sochi, unatarajiwa kuwa mwendelezo wa mazungumzo ya awali katika mkutano wa kilele wiki iliyopita mjini Tehran, Iran. Kwenye mkutano huo, Putin alipuuzilia mbali pendekezo la Erdogan la usitishwaji kamili wa mapigano kwenye jimbo hilo la Idlib.

Awali, kabla ya mazungumzo yao, rais Erdogan aliwaambia waandishi wa habari kwamba mkutano huo wa Sochi utaibua matumaini mapya katika ukanda huo, ingawa hakuonyesha kiashiria chochote kuhusu kile watakachokwenda kukizungumza watakapotoa taarifa yao ya pamoja baada ya mkutano.

Uturuki inayowaunga mkono waasi wa Syria wanaompinga rais Bashar al-Assad, amekuwa akifanya mazungumzo na washirika wake Urusi na Iran kuhusu mustakabali wa jimbo la Idlib linalodhibitiwa na waasi nchini Syria, pamoja na maeneo yanayolizunguka ambayo Assad ameapa kuyarejesha.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/DPAE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef