1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin kuamua kuhusu hatma za dhamana za usalama

27 Desemba 2021

Rais wa Urusi amesema atatafakari kuhusu maamuzi ya kuchukuwa iwapo mataifa ya Magharibi yatashindwa kutimiza matakwa yake ya dhamana ya usalama yanayojumuisha sharti la kutoiruhusu Ukraine kujiunga na NATO.

https://p.dw.com/p/44raY
Russland I Präsident Putin
Picha: SPUTNIK/REUTERS

Rais Putin ameyahimiza mataifa hayo kuchukuwa hatua za haraka kutoa hakikisho hilo na kuonya kuwa taifa lake litalazimika kuchukuwa hatua mwafaka za kijeshi na kiteknolojia iwapo mataifa hayo yataendelea na alichokiita, ''visa vya uchokozi'' katika eneo hilo.

Kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali ya Urusi jana kilipeperusha majibu ya Putin kuhusu hatua zitakazochukuliwa na taifa hilo iwapo masharti yake hayatatimizwa ambapo alisema kuwa itategemea mapendekezo yatakayowasilishwa kwake na wataalamu wa kijeshi.

Marekani na washirika wake, wamekataa kutoa aina ya dhamana anayotaka Putin kuhusu Ukraine na kutaja kanuni ya NATO kuwa uanachama uko wazi kwa nchi yoyote inayokidhi viwango.