1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin azitaka Armenia na Azerbaijan kujizuia na mapigano

20 Septemba 2022

Rais wa Urusi Vladmir Putin amesema nchi yake ina wasiwasi kuhusu mapigano mapya yaliyozuka kati ya Armenia na Azerbaijan, akitoa wito kwa maadui hao wa kihistoria kuzungumza na kusuluhisha mgogoro wa eneo wanalozozania.

https://p.dw.com/p/4H7FP
Aserbaidschans Armeestation in der Stadt Lachin
Picha: Resul Rehimov /AA/picture alliance

Akizungumza Jumanne kwa njia ya televisheni, Putin amesema anataka kusisitiza kwamba hali zote za migogoro kati ya nchi hizo jirani zinawaletea na wao pia wasiwasi.

Mapigano yalizuka wiki iliyopita kati ya mataifa hayo mawili na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 200. Vita vya wiki sita vilimalizika huku zaidi ya watu 6,500 wakiwa wameuawa na makubaliano ya amani ya Urusi, huku nchi hiyo ikipeleka maelfu ya wanajeshi wa kulinda amani.

"Tunatoa wito kwa kila mmoja kujizuia, kuzingatia kwa dhati mpango wa kusitisha mapigano na kufuata taarifa za pande tatu za viongozi wa Urusi, Azerbaijan na Armenia," alisisitiza Putin.

Putin azungumza baada ya mkutano wa wanadiplomasia

Putin ameutoa wito huo baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken siku ya Jumatatu kuhimiza uwepo wa amani kati ya mahasimu hao wakubwa, wakati alipowakutanisha pamoja wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa nchi hizo mbili kwa mara ya kwanza tangu yalipozuka mapigano makali katika mpaka wa nchi zao mapema mwezi huu.

Blinken alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Armenia, Ararat Mirzoyan na Waziri wa Mambo ya Nje wa Arzerbaijan, Jeyhun Bayramov mjini New York, Marekani hayo yakiwa mazunguzo ya moja kwa moja kati ya viongozi hao, pembezoni mwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Katika mkutano huo, Blinken alitoa salamu za rambirambi kwa wote waliopoteza maisha na kusisitiza umuhimu wa kuzuia uhasama zaidi, na umuhimu wa kurejea katika mchakato wa amani.

US-Außenminister Antony Blinken trifft sich in New York mit dem ägyptischen Außenminister Sameh Shoukry
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken akikutana na ujumbe wa Armenia akiwemo Waziri wake wa Mambo ya Nje, Ararat Mirzoyan, na ujumbe wa Azerbaijan akiwemo Waziri wake wa Mambo ya Nje, Jeyhun Bayramov,New York, MarekaniPicha: Craig Ruttle/REUTERS

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Ned Price, viongozi hao watatu pia walijadiliana hatua zinazofuata na Blinken akazihimiza pande zote mbili kukutana tena kabla ya mwisho wa mwezi.

Katika mkutano huo wa Jumatatu, Waziri Mirzoyan alivitolea wito vikosi vya jeshi vya Azebaijan kuondoka katika ardhi ya Armenia na "utaratibu wa kimataifa" uanzishwe kwa ajili ya kuzuia mapigano zaidi.

Azerbaijan iko wazi kwa mazungumzo

Wakati huo huo, Waziri Bayramov alisema kabla ya mkutano huo kwamba nchi yake imeridhishwa na kiwango cha uhusiano na Marekani na kuongeza kuwa mazungumzo yake ya moja kwa moja na Mirzoyan hayakuwa ya kawaida. Alisema siku zote wako tayari kwa mikutano.

Ama kwa upande mwingine, wakati wa ziara yake ya Yerevan mwishoni mwa juma lililopita, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi aliishutumu Arzebaijan kwa mashambulizi yasiyo halali nchini Armenia na kulaani shambulizi dhidi ya uhuru wa nchi hiyo.

Kuongezeka kwa ushirikiano wa kidiplomasia wa Marekani kunaipa changamoto nafasi ya Urusi kama mpatanishi mkuu wa ukanda huo, huku kukiwa na hali ya wasiwasi nchini Armenia kutokana na kukosa kuungwa mkono na mshirika wake wa jadi, Urusi, ambao umeharibiwa na vita vyake nchini Ukraine.

(AFP, DW https://bit.ly/3LuIDUd)