Putin asema Warusi wengi wanamuunga mkono kubadilisha katiba
12 Juni 2020Rais wa Urusi Vladmir Putin amesema Warusi wengi zaidi wameunga mkono mpango wake tata wa mabadiliko ya katiba ili kumpa mwanya wa kubakia madarakani.
Putin amesema hayo mnamo Juni 12 alipohudhuria hafla ya ''siku ya Urusi'' nchini humo. Akionekana hadharani kwa mara ya kwanza, tangu Urusi, nchi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya maambukizi ya Corona kuwekwa chini ya vizuizi vya kuzuia Covid-19, Putin amesema idadi kubwa ya raia nchini humo wanakubaliana na kiongozi huyo kuhusu mpango huo ambao huenda utamwezesha kiongozi huyo mwenye miaka 67 kusalia katika usukani wa nchi hiyo.
Putin alionekana akiwasalimia maafisa wake wakati wa sherehe ziliziofanyika maghharibi mwa Moscow, mji mkuu wa Urusi.
Bila kuvalia barakoa, huku akizungukwa na washirika wake,Putin alionekana akitabasamu na kuwapongeza wanainchi kwa moyo wao wa uzalendo pamoja na kulinda mila na utamaduni wao.
Putin ambaye ameitawala siasa za Urusi kwa miungo miwili mnamo Januari alizindua mpango wa kutaka kubadilisha katiba. Endapo mpango huo utafua dafu itakuwa mara ya kwanza kwa sheria mama katika katiba ya nchi hiyo kufanyiwa marekebisho tangu mwaka 1993.
Wakati huo huo, Urusi nchi ya tatu duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi wa Covid-19, katika siku za hivi karibuni imeanza kulegeza vizuizi hivyo huku taifa hilo likielekea kupiga kura mnanmo Julai mosi, kura ambayo wachambuzi wanasema huenda ikamsafishia Putin njia ya kubakia madarakani hadi ifikapo mwaka 2036.
Ijapokuwa visa vya maambukizi vimekuwa vikishuka nchini humo, maafisa wa afya na wakosoaji wa serikali wameonya kuwa bado ni mapema mno kuondoa vizuizi hivyo hasa katika mji wa Moscow, ambao ndio kitovu cha COVID-19. Wakosoaji wanamshutumu Putin kwa kuharakisha kulegeza vizuizi kwa maslahi binafsi.
Hadi kufikia Juni 12, Urusi ilirekodi visa vipya 8,987 vya mambukizi ya Covid 19 na hivyo idadi jumla ya visa kufikia 511,423, huku Moscow, mji wenye idadi kubwa zaidi ya wakaazi barani Ulaya ukiwa na watu milioni 12, mnamo siku hiyo hiyo ulithibitisha visa vipya 1,714.
Chanzo: AFPE