1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pritoria. Afrika kusini kuisaidia Zimbabwe kulipa deni.

25 Julai 2005
https://p.dw.com/p/CEqt

Rais wa Afrika kusini Bwana Thabo Mbeki amesema kuwa nchi yake huenda ikachukua baadhi ya deni la kigeni la Zimbabwe.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Pritoria, Mbeki amesema kuwa mazungumzo yanaendelea na serikali ya rais Robert Mugabe.

Amesema kuwa Afrika kusini inataka kuzuwia kuanguka kwa uchumi wa Zimbabwe na inaweza ikachukua sehemu ya deni inalodaiwa Zimbabwe linalofikia dola za Kimarekani bilioni 4.5.

Zimbabwe inapambana na mzozo mkubwa wa kiuchumi tangu kupata uhuru kutoka Uingereza mwaka 1980.

Ripoti za vyombo vya habari zimesema wiki iliyopita kuwa Zimbabwe imeomba mkopo wa dola bilioni 1 za kununulia chakula na mafuta na kuzuwia kuondolewa kutoka katika shirika la fedha la kimataifa IMF, kutokana na kulimbikiza malipo ya dola milioni 300.

Wakati huo huo rais Robert Mugabe amewasili mjini Beijing, nchini China leo katika juhudi za kupata mkopo na vitega uchumi kwa uchumi wa nchi yake unaoporomoka, bila masharti.

Bwana Mugabe analaumu vikwazo vilivyowekwa na mataifa ya magharibi kuwa ndivyo vinavyoharibu hali uchumi wa nchi yake kutokana na zoezi la kuchukua mashamba ya wazungu na kuwapa raia wa Kiafrika katika nchi hiyo.