Prabowo Subianto ashinda uchaguzi wa urais Indonesia
21 Machi 2024Tume ya uchaguzi ya Indonesia imetangaza kuwa Subianto, aliyekuwa waziri wa ulinzi na mgombea mwenza wake Gibran Rakabuming Raka, walipata zaidi ya kura milioni 96 ambayo ni sawa na asilimia 59 ya kura katika uchaguzi huo uliofanyika Februari 14.
Wapinzani wake, aliyekuwa gavana wa Jakarta Anies Baswedan alipata asilimia 24.9 ya kura huku gavana wa zamani wa jimbo la Java ya Kati Ganjar Pranowo akijikingia zaidi ya asilimia 16 ya kura.
Soma pia: Mgombea urais Indonesia kupinga matokeo mahakama ya katiba
Zaidi ya watu milioni 164 walishirika zoezi hilo la kura, idadi hiyo ikiwa ni takriban asilimia 80 ya watu wote waliojiandikisha kama wapiga kura.
Prabowo, kamanda wa zamani wa kikosi maalum cha ulinzi na ambaye anatuhumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu, atachukua nafasi ya rais anayeondoka Joko Widodo mnamo mwezi Oktoba baada ya kukamilika kwa kipindi cha mpito.