1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Papa Francis alaani shambulizi la Moscow

24 Machi 2024

Kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis amewaombea wahanga wa shambulizi la watu waliokuwa kwenye tamasha mjini Moscow, akilitaja kama uasi na kitendo kisicho cha kibinaadamu chenye kumchukiza Mungu.

https://p.dw.com/p/4e4X0
Vatican City | Papa Francis akiongoza sala
Papa Francis ameongoza ibada ya Matawi kwa kuwaombea wahanga wa shambulizi la mjini Moscow, huku akililaani na kusema ni chukizo kwa MunguPicha: Alessandra Tarantino/AP/dpa/picture alliance

Papa Francis amesema hayo wakati wa Ibada ya Matawi katika Kanisa la Mtakatifu Petro, wakati Urusi ikiwa inafanya maombolezo ya kitaifa hii leo ya kuwakumbuka wahanga wa shambulizi hilo lililosababisha vifo vya watu 137 hadi sasa.

Papa Francis ambaye aliongoza ibada hiyo mbele ya umati wa watu wa Vatican uliokadiriwa kufikia 25,000, hata hivyo alizungumza kwa sauti dhaifu na hakutoa hotuba yake kama ilivyopangwa.

Mwezi uliopita kiongozi huyo aliugua mafua na tangu hapo amekuwa akiwaomba watu wengine kumsomea hotuba yake.

Ibada hii ya Liturujia inaashiria mwanzo wa Wiki Takatifu, ambapo Papa anaongoza mfululizo wa matukio muhimu kuelekea Pasaka, sikukuu muhimu zaidi kwa Wakristo.