1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi ya Misri yaahirisha msako

14 Agosti 2013

Wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani na jeshi nchini Misri Mohammed Mursi wamekaidi amri ya kuwataka waondoke katika viwanja viwili wanakofanyia maandamano mjini Cairo

https://p.dw.com/p/19OSc
CAIRO, EGYPT - AUGUST 12: Supporters of deposed Egyptian President Mohammed Morsi perform morning prayer at sunrise during a sit-in demonstration near the Rabaa al-Adweya Mosque in the Nasr City district on August 12, 2013 in Cairo, Egypt. Egyptian security forces threatened to begin a siege of pro-Morsi protest camps in Cairo overnight on August 11, however Egypt's Interior Ministry appeared to have put off plans to crack down on protesters early on Monday. Morsi supporters have continued to protest at sites across Cairo over one month after the Egyptian military deposed Egypt's first democratically elected President, Mohammed Morsi, on July 3. (Photo by Ed Giles/Getty Images).
Ägypten Mursi Anhänger 12. August 2013Picha: Getty Images

Waandamanaji hao wanasema watakabiliana na polisi watakaojaribu kuwaondoa kwa kutumia mawe na imani yao. Wakati huo huo Marekani imeitaka serikali ya mpito ya Misri kuacha kuwakamata na kuwazuia watu kwa sababu za kisiasa.

Kufikia jana usiku, mitaa ya mji mkuu Cairo ilikuwa na utulivu, baada ya vikosi vya usalama kuahirisha hatua za kuwaondoa waandamanaji, licha ya kutoa ilani mwishoni mwa wiki kwamba vilikuwa tayari kuvunja kambi za maandamano, kwa nguvu ikibidi. Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni Nabil Fahmy amesema kila juhudi inafanywa kuhakikisha kuwa suluhisho linapatikana kupitia mazungumzo.

Wafuasi wa Mursi wanadai arejeshwe madarakani
Wafuasi wa Mursi wanadai arejeshwe madarakaniPicha: picture-alliance/AP Photo

Na katika mwelekeo mwingine wa kisiasa, chama cha Al Nour kimesema kitajiunga na jopo la bunge linaloandika katiba mpya, na kuunga mkono kipindi cha mpito cha kisiasa kinachosimamiwa na jeshi, baada ya mapinduzi ya Mursi mwezi uliopita. Al-Nour ni chama cha pili kwa ukubwa kinachofuata nadharia za kiislamu, baada ya kundi la udugu wa Kiislamu la kile cha Mursi, cha Udugu wa Kiislamu.

Katika kambi ya al-Nahda, inayopatikana katikati mwa jiji la Cairo, hali ilikuwa tulivu, na mwandamanaji mmoja alipoulizwa kuhusu hatua ya kijeshi, alisema, na namnukuu, “walisema hivyo siku 15 zilizopita”. “Kila mara wao husema watayavunja maandamano”

Chama cha Udugu wa Kiislamu kinasema kuwa kuangushwa Mursi, ambaye alishidna uchaguzi rais wa kwanza ulioandaliwa kidemokrasia nchini humo, ni pigo kubwa kwa uhalali wa sheria. Wanadai kuwa hawaondoki makambini hadi pale atakaporejeshwa madarakani. Gehad El-Haddad ni msemaji wa Udugu wa Kiislamu. "Lengo hapa siyo mkusanyiko, lengo ni nini wanachokitaka watu. Watawanya kundi moja, watakusanyika tena. Maandamano haya yataendelea, yanashika kasi, yanaingia katika mioyo na mawazo ya watu na yataendelea hadi jeshi litakapobadlisha uamuzi wa kuipundua utawala wa Mursi."

Mkuu wa jeshi la Misri Jenerali Abdel Fattah al-Sisi
Mkuu wa jeshi la Misri Jenerali Abdel Fattah al-SisiPicha: Reuters

Jeshi liliahirisha hatua ya kuwafurusha likihofia kuzuka kwa machafuko na umwagikaji damu. Mkuu wa Jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Sisi anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa maafisa wenye msimamo mkali kuyavunja maandamano hayo. Lakini wajumbe wa nchi za Magharibi na Kiarabu pamoja na baadhi ya maafisa wa serikali ya Misri wanalishinikiza jeshi lisitumie nguvu.

Waziri wa mambo ya Kigeni Abdel Fahmy anasema haki ya kufanya maandamano ya amani itaheshimiwa. Lakini akadokeza kuwa kutakuwa na kiwango ambacho serikali inaweza kuvumilia. Afisa mmoja wa usalama amesema waandamanaji wataondolewa hatua kwa hatua. Ilani zitatolewa na polisi watatumia mabomba ya maji kuwatawanya wale watakaokataa kusalimu amri.

Marekani hapo jana imewataka viongozi wapya wa Misri wasitishe “ukamataji na uzuiaji wowote wa watu unaochechewa kisiasa”, ijapokuwa haikutaja chochote kuhusiana na mstakabali wa rais aliyepinduliwa Mohammed Mursi. Naibu msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Marie Harf amesema kuendelea kuwazuilia watu kizuizini ni mojawapo ya matatizo ambayo Misri inastahili kuyatatua kivyake kama ingetaka kusonga mbele kutokana na mkwamo wa kisiasa ambao umedumu kwa siki sita sasa.

Mwandishi: Bruce Amani/reuters

Mhariri: Gakuba Daniel