1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaArgentina

Polisi wapambana na waandamanaji wapinga mageuzi Argentina

13 Juni 2024

Mamia ya polisi wa kutuliza fujo wametumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji kwenye mji mkuu wa Argentina, Buenos Aires.

https://p.dw.com/p/4gyW7
Maandamano ya umma Argentina.
Mapendekezo ya maguezi ya kiuchumi yanapingwa na umma nchini Argentina. Picha: Roberto Almeida Aveledo/ZUMA/picture alliance

Mamia ya watu waliteremka mitaani kupinga mapendekezo ya mageuzi ya kiuchumi yaliyotangazwa na serikali.

Magari mawili yalitiwa moto na waandamanaji wenye hasara pale maandamano hayo ya umma yalipogeuka kuwa ya vurugu. Vurumai hiyo imetokea katika wakati wabunge wa nchi hiyo wanajadili mapendekezo ya mageuzi mapana ya kiuchumi yaliyowasilishwa na Rais Javier Milei.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuzifuta idara kadhaa za serikali, kubinafsisha kiasi dazani ya mashirika ya umma ikiwemo kampuni ya ndege ya taifa na kupunguza mafao ya wastaafu na kulegeza masharti yanayotoa ulinzi kwa watu walioajiriwa.

Wanasiasa wa mrengo wa shoto na vyama vya wafanyakazi wanayapinga mageuzi hayo wakisema yatalirejesha nyuma taifa hilo. Hata hivyo utawala wa Milei unasisitiza mageuzi hayo ni ya lazima ili kuufufua uchumi wa Argentina unaokabiliwa na msukosuko.