Polisi wa Kenya washika doria katika mji mkuu wa Haiti
18 Julai 2024Polisi wa Kenya walishika doria katika mji mkuu wa Haiti huku wakiwa na magari ya kivita jana Jumatano, ikiwa ni siku moja tu baada ya kuwasili kwa askari wengine wa nyongeza 200 kutoka katika taifa hilo la Afrika Mashariki, ikiwa ni sehemu ya juhudi ya nchi hiyo ya kufanikisha usalama Haiti.
Duru zilisema magari hayo yameonekana kufanya doria katika maeneo yanayozunguka Ikulu ya Kitaifa na maeneo mengine ya Port-au-Prince yakiwa na wanajeshi wa Kenya wakishirikiana na polisi wa Haiti.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ufaransa AFP, vishindo kadhaa vilisikika wakati magari hayo yakipita, ingawa haikufahamika mara moja kama ni risasi zilizofyatuliwa na polisi au magenge yenye silaha ambayo yanadhibiti takriban asilimia 80 ya mji mkuu, Port-au-Prince.
Hadi wakati huu Kenya imewapeleka takriban askari 400 nchini Haiti, 200 Juni 25 na 200 siku ya Jumanne huku kukiwa na ahadi ya wengine 600 katika majuma yajayo.