1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Ujerumani yachunguza shambulizi la kisu

27 Juni 2021

Uchunguzi wa polisi kuhusu shambulizi hatari la kisu katika mji wa kusini mwa Ujerumani wa Wuerzburg umetoa matokeo ya mwanzo, wakati umma ukiendelea kukumbwa na mshtuko

https://p.dw.com/p/3vcnZ
Deutschland Würzburg l Polzeiaufgebot Nach Messerattacke
Picha: Michael Probst/AP/picture alliance

Uchunguzi wa polisi kuhusu shambulizi hatari la kisu katika mji wa kusini mwa Ujerumani wa Wuerzburg umetoa matokeo ya mwanzo, wakati umma ukiendelea kukumbwa na mshtuko. Watu watatu waliuawa katika duka moja katikati mwa mji wa Wuerzburg Ijumaa na wote walikuwa wanawake, polisi imesema katika kikao cha waandishi wa habari. Sita kati ya watu saba waliojeruhiwa pia walikuwa wanawake, mmoja akiwa kijana wa kiume.

Deutschland Würzburg l Gedenken nach der Messerattacke
Wakaazi bado wana mshtuko kufuatia shambuliziPicha: Michael Probst/AP/picture alliance

Polisi imesema haijawa wazi kama mtuhumiwa wa shambulizi hilo, mhamiaji mwenye umri wa miaka 24, aliwalenga wanawake kwa makusudi au kama ilikuwa kwa bahati mbaya. Mara tu kabla ya shambulizi hilo, mshambuliaji huyo aliomba visu dukani humo, kisha akachukua kimoja na kumchoma muuzaji na kumjeruhi vibaya. Kisha akawauwa wanawake wawili wengine dukani hapo kabla ya kuwashambulia watu katika benki iliyokaribu.

Nia ya shambulizi bado haijajulikana

Nia ya mtuhumiwa huyo, ambaye aliwachoma kisu kiholea wapita njia na bila kutoa onyo, bado haijulikani. Polisi mmoja alimpiga risasi mguuni lakini hakutarasisha maisha yake.

Mshukiwa huyo, anayesemekana kuwa Ujerumani kwa karibu miaka mitano na kupewa hadhi ya ulinzi, alikuwa tayari anafahamika kwa polisi kabla ya shambulizi hilo. Wapelelezi walikuta ujumbe wa chuki katika kituo cha wasio na makazi alichoishi mara ya mwisho. Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Upelelezi Armin Kuehnert amesema walikuta ujumbe kwenye simu yake ambao utafanyiwa uchunguzi.

Deutschland Kriminalität l Nach der Messerattacke in Würzburg
Duka ambalo mshambuliaji alichukua kisu Picha: Michael Probst/AP/picture alliance

Kwa mujibu wa polisi, mwanaume huyo awali alipewa matibabu ya kiakili, baada ya kuhusika katika ajali kituo cha wasio na makaazi Januari ambapo aliwatishia wenzake na kisu. 

Alisema Allahu Akbar

Nia ya itikadi kali pia inachunguzwa kwa sababu mshukiwa huyo anadaiwa kusema kwa sauti kubwa "Allahu Akbar" kumaanisha "Mungu ni Mkubnwa" katika Kiarabu, wakati wa shambulizi hilo.

Kwa mujibu wa wakili wake, mshukiwa huyo sasa anakabiliwa na mashitaka matatu ya mauaji na sita ya kujaribu kuuwa.

Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria Markus Soeder amesema matukio hayo hayawezekani na ni ya kushtusha, akiongeza kuwa Bavaria inaomboleza na kila mmoja kwa mkasa huo. 

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema mshambuliaji huyo alitumia ukatili mkubwa na atakabiliwa na mkondo wa sheria.

DPA