1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Burundi yaonya kuhusu uhasama wa vyama kwenye kampeni

Amida ISSA/ Bujumbura29 Aprili 2020

Kwenye siku ya 3 ya kampeni ya uchaguzi Burundi, polisi nchini huo imesema kuna hali ya uhasama na visa vya chokochoko kati ya vyama vya Cndd Fdd na CNL.

https://p.dw.com/p/3bZCt
Brundi | Generalmajor Ngayihimiye Évariste
Picha: DW/A. Niragira

Hayo ni wakati mgombea wa chama tawala Evariste Ndayishimiye ameendesha kampeni yake katika mkoa wa Muramvya, na Jana alikuwa katika tarafa ya Kayokwe mkoa wa Mwara eneo la kuzaliwa rais Merchiol Ndadaye. Naye mgombea wa CNL Agathon Rwasa leo yu muyinga kwenye mpaka na Tanzania, akibaini kuwa ukiukaji sheria uko wazi katika kampeni hii.

Mgombea Evariste Ndayishimiye wa chama Cndd Fdd anaendelea na kampeni akiwa tayari amepata uungaji mkono kutoka vyama vya 27 vya siasa.  Meya wa Jiji la Bujumbura Fredd Mbonimba amewashangaza wengi kwa kutangaza kuwa yeye na familia yake watampigia kura mgombea wa chama tawala.

Mgombea wa chama cha CNL Agathon Rwasa
Mgombea wa chama cha CNL Agathon RwasaPicha: E. Ngendakumana

Evariste Ndayishimiye ameendesha kampeni katika mkoa wa Muramvya, baada ya kurindima katika tarafa ya Kayokwe mkoani wa Mwaro, eneo la kuzaliwa Hayati rais Merchiol Ndadaye wa kwanza kuchaguliwa chini ya misingi ya kidemokrasia. Mgombea huyo wa chama tawala ameahidi kuwafikishia maendeleo wananchi.

"Ninaahidi kuwa nitaweka kipaumbele katika sekta zinazozalisha. Tunajuwa kuwa kilimo kinaendeshwa na wengi ya raia wa hapa. Tutaongeza mimeya ili ipatikane kwa wingi na kuuzwa nje ya nchi na hivyo nchi yetu iweze kuingiza pesa za kigeni zitakazotuwezesha kupatikana vile visivyotengenezwa hapa." Amesema Evariste.

Rais anayetarajiwa kuondoka madarakani Pierre Nkurunziza (aliyeinua mkono juu)
Rais anayetarajiwa kuondoka madarakani Pierre Nkurunziza (aliyeinua mkono juu)Picha: E. Ngendakumana

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza ameendelea kudhihirisha uungaji wake mkono kwa mrithi wake. Wakiwa bega kwa bega tangu kuanza kampeni, rais Nkurunziza amewataka wafanyakazi kuwa makini ili kusiwepo na watakaopora mali ya umma na hivyo mrithi wake akute hazina ya serikali ikiwa tupu.

Mgombea wa chama Uprona Gaston Sindimwo anaendesha kampeni yake jijini hapa Bujumbura huku akionekana kutowavutia watu wengi, baada ya baadhi ya wafuasi wa chama chake Uprona kuamuru kumpigia kura Evariste Ndayishimiye.

Chama mashuhuri cha upinzani CNL kimeendesha leo kampeni katika mkoa wa Muyinga. Mgombea wake Agathon Rwasa ameiambia DW, mmoja na wafuasi wake aliuwawa na wengiune kukamatwa, na kwamba ukiukaji sheria uko wazi lakini wameamuwa kusonga mbele.

Polisi Burundi yasema kuna uhasama kati ya vyama vya siasa wakati kampeni ikiendelea
Polisi Burundi yasema kuna uhasama kati ya vyama vya siasa wakati kampeni ikiendeleaPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Polisi ya taifa tayari imekemea mienendo iliyoitaja kuwa mibovu katika kampeni hii. Pierre Nkurikiye msemaji wa polisi amesema tayari kumeshuhudiwa hali ya uhasama na visa vya chokochoko kati ya vyama vya Cndd Fdd na CNL.

Naye mkuu wa tume ya kitaifa ya haki za binaadam Sixte Vigny Nimuraba amewataka wanasiasa kutumia busara na kuepuka kufufua chuki za kisiasa nchini.

Kampeni hii itamalizika Mei 17 huku uchaguzi wa rais, bunge na ule wa madiwani ukipangwa kunyika Mi 20.