1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Berlin yavunja maandamano dhidi ya vizuizi vya corona

Sekione Kitojo
29 Agosti 2020

Polisi mjini Berlin ilivunja maandamano makubwa katika mji huo mkuu wa Ujerumani yaliyoitishwa kupinga vizuizi vya virusi vya corona saa chache tu baada ya kuanza. Taklriban waandamanji 18,000 walikusanyika mjini humo

https://p.dw.com/p/3hk0A
Deutschland Berlin Protest gegen Corona-Maßnahmen
Picha: Reuters/C. Mang

Hii ni baada ya waandamanaji kushindwa kuzingatia maagizo ya kutosogeleana na kuvaa maski. Maandamano hayo yamekuja wakati maambukizi yakiongezeka Ulaya na wakati hasira ya umma kuhusu hatua za kudhibiti virusi hivyo ikiongezeka katika baadhi ya maeneo. Matukio sawa na ya Berlin yalitokea Paris, London na kwingineko leo.

Karibu polisi 3,000 waliwekwa katika mitaa ya Berlin kuudhibiti umati wa watu karibu 18,000. Waandamanaji walitayanyika kwa amani ijapokuwa kulikuwa na baadhi waliozusha vurugu. Polisi walikuwa wamejiandaa kwa uwezekano wa kuzuka vurugu baada ya wanaharakati wanaopinga hatua za kudhibiti virusi hivyo kuwahimiza wafuasi wao kwenye mitandao ya kijamii kote Ulaya kujihami na kukusanyika mjini Berlin.

Deutschland Berlin Protest gegen Corona-Maßnahmen
Kulikuwa na matukio kadhaa ya vuruguPicha: Reuters/A. Schmidt

Maafisa wa mji wa Berlin awali waliamua kutoyaruhusu maandamano hayo ya leo, wakihofia kuwa idadi inayokadiriwa ya waandamanaji 22,000 hawatazingatia masharti ya kukaa umbali wa mita moja na nusu au kuvaa barakoa. 

Lakini katika mkesha wa maandamano hayo, mahakama ya Berlin iliwaunga mkono waandamanaji, ikisema hakuna dalili kuwa waandalizi watapuuza makusudi kanuni hizo na kuhatarisha afya ya umma. Mpaka sasa, Ujerumani imemudu kulishughulikia janga la corona kuliko nchi nyingine za Ulaya, kwa kutekeleza mpango wa upimaji wa watu wengi ili kupunguza idadi ya maambukizi na vifo.

Lakini idadi ya maambukizi ya kila siku imeongezeka katika wiki za karibuni, kama tu ilivyo katika maeneo mengine duniani. Siku ya Ijumaa, Kansela Angela Merkel aliwahimiza wananchi kuwa waangalifu dhidi ya kirusi hicho.

Waandamanaji walikusanyika mbele ya Lango la Brandenburg katikati ya Berlin kabla ya maandamano hayo wakiwa na mabango yenye ujumbe wa "Komesheni Uwongo wa corona" na "Merkel lazima aondoke"

Karibu wanaharakati wengine 200 wanaopinga uvaaji barakoa waliandamana Paris wakiwa na ujumbe kama vile "Waache watoto wetu wapumue".

Mjini Lomdon, mamia kadhaa ya waandamanaji walikusanyika katika uwanja wa Trafalgar wakiliita janga la corona kuwa "utapeli” na kudai kuondolewa kwa vizuizi. Virusi hivyo vimewauwa Zaidi ya watu 40,000 nchini Uingereza.

reuters