1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi 20 Kenya wameuawa ama walijiua tangu Januari 2021

Shisia Wasilwa26 Oktoba 2021

Takwimu za Shirika Huru la Kutetea Haki za waathiriwa Kisheria na Kimatibabu la IMLU nchini Kenya zinaonesha kuwa maafisa 20 wa polisi wameuawa ama walijiua tangu mwezi Januari mwaka 2021. Shisia Wasilwa anaripoti zaidi.

https://p.dw.com/p/42Bgn

Shirika hilo linasema kuwa vifo hivyo vimetokana na matatizo ya afya ya akili, hali inayoibua wasiwasi miongoni mwa maafisa hao walio na jukumu la kudumisha amani na utangamano.

Ripoti ya shirika la IMLU inajiri huku visa vya maafisa wa polisi kuuana au kujiua vikizidi kushuhudiwa katika pembe mbali mbali za taifa la Kenya. Shirika hilo, linasema kuwa, juhudi kubwa zinafanywa kuwawaajibisha maafisa wa polisi waliopotoka bila ya kuzinguatia afya zao za akili.

Baadhi ya changamoto wanazokabiliwa nazo, zimesababishwa na asili ya kazi zao huku nyingine zikichangiwa na matatizo ya maisha. Ripoti hiyo inaeleza kuwa, maafisa hao wanahitajika kudumisha sheria na utangamano katika mazingira magumu, hivyo kuhatarisha maisha yao, kila siku wanapoamka. Caroline Tunen ni afisa wa mipango wa shirika la IMLU anafafanua.

“Maafisa 21 wamejiua ama wameua wenzao, kutoka mwezi Januari, hiyo ni idadi kubwa na tunajua kwa idara ya polisi imeweka mikakati ya kuangazia suala hilo abalo ni la dharura,” amesema Tunen.

Mauaji ya Konstebo John Ogweno, aliyekuwa na umri wa 28, na Coroline Kangogo anayedaiwa kuwa mpenzi wake mwezi Julai, ni ukumbusho wa jinsi afya ya akili miongoni mwa maafisa wa vikosi vya kudumisha amani ni suala nyeti.

Kangogo aliua mtu mwingine katika jimbo la Kiambu alipokuwa akitoroka mamlaka. Baadaye inadaiwa alijitoa uhai kwa kujipiga risasi nyumbani kwake Iten. George Musamali ni mtaalamu wa masuala ya usalama.

Ripoti ya shirika la IMLU inajiri huku visa vya maafisa wa polisi kuuana au kujiua vikizidi kushuhudiwa katika pembe mbali mbali za taifa la Kenya.
Ripoti ya shirika la IMLU inajiri huku visa vya maafisa wa polisi kuuana au kujiua vikizidi kushuhudiwa katika pembe mbali mbali za taifa la Kenya. Picha: Reuters/T. Mukoya

”Mchango mkubwa kwa hali hii unatokona na mazingira ya utendajikazi wa polisi, halikadhalika masuala ya kijamii, ambayo huwashinikiza kutenda visa vya kutisha, ijapokuwa wao ndio walinda usalama,” amesema Musamali.

IMLU inasema kuwa baadhi ya viashiria vinavyochangia msongo wa mawazo, kujitoa uhai na hata kuuana miongoni maafisa wa polisi nchini Kenya ni mzigo ambao jamii imewawekea maafisa hao kuwa wanastahili kutatua masuala yote ya kiusalama.

Aidha visa vinne zaidi vya mauaji vimeripotiwa mwezi huu ambavyo havijanakiliwa hivyo kufanya idadi iliyotolewa kuwa juu zaidi. Gacheke Gachuhi ni mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu na hapa analaani mauaji ya kiholela yanayodaiwa kutekelezwa na maafisa wa polisi.

“Mauaji yanatokea kila siku, na polisi wanahusika, hii pia inawadhuru afya zao kiakili,” amesema Gacheke.

Mnamo Juni mwaka huu, Wizara ya Afya nchini Kenya ilizindua Mpango wa Utekelezaji wa Afya ya Akili Kenya ya miaka mitano kuanzia mwaka ujao. Aidha kuna mswada wa marekebisho wa Afya ya Akili katika bunge la Seneti huku wito wa pamoja kutoka kila pembe ukinuia kutangaza tatizo hili kuwa janga la taifa.