1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poland, Bulgaria zakatiwa gesi ya Urusi

Admin.WagnerD27 Aprili 2022

Ukraine imeituhumu Urusi kuwa inaihujumu Ulaya kwa kusitisha usambazaji wa gesi nchini Poland na Bulgaria wakati mzozo nchini Ukraine ukiendelea kutokota. Nchi hizo zimekataa kulipia gesi katika sarafu ya Kirusi ya ruble

https://p.dw.com/p/4ATjI
Ukraine Gaspipeline (2008)
Picha: Sergey Dolzhenko/dpa/picture-alliance

Poland, ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na mkosoaji mkubwa wa Urusi ni miongoni mwa nchi za Ulaya zinazotafuta vikwazo vikali zaidi dhidi ya Urusi kwa uvamizi wake. Mwanachama mwenza wa NATO Bulgaria inategemea pakubwa gesi ya Urusi.

Kampuni ya gesi ya Poland inayomilikiwa na serikali PGNiG imesema usambazaji wa gesi kutoka kampuni kubwa ya nishati ya Gazprom kupitia Ukraine na Belarus utasitishwa leo asubuhi, lakini Warsaw imesema wateja wake hawapaswi kuwa na wasiwasi kwa sababu hifadhi yake ya gesi ni asilimia 76.

Rais wa Urusi Vladmir Putin amezitaka nchi anazoziita zisizo za kirafiki kulipia bidhaa za gesi katika sarafu ya rouble, hatua ambayo ni wanunuzi wachache tu ndio wameitekeleza mpaka sasa. 

Andriy Yermak, mkuu wa utumishi katika ofisi ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Urusi inajaribu kuuvunja umoja wa washirika wa Ukriane kwa kutumia raslimali za nishati kama silaha.

Krauss Maffei Wegmann Flugabwehrkanonenpanzer Gepard
Ujerumani kupeleka Ukraine vifaru aina ya GepardPicha: Peter Steffen/picture-alliance

Mapigano yaendelea

Wakati huo huo, mapigano yanaendelea mashariki na kusini mwa Ukraine. Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema wanajeshi wake "wamelikomboa jimbo lote la Kherson kusini mwa Ukraine na sehemu za majimbo ya Zaporizhzhia, Mykolaiv na Kharkiv. Kama taarifa hizo zitadhibitishwa, zitaashiria mafanikio muhimu kwa upande wa Urusi katika vita hivyo.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin, akiwakaribisha maafisa kutoka zaidi ya nchi 40 katika Kituo cha Jeshi la Angani cha Ramstein nchini Ujerumani, ambacho ni makao makuu ya jeshi la angani la Marekani barani Ulaya, amesema "mataifa kote ulimwenguni yanasimama pamoja katika kuiunga mkono Ukraine na katika vita vyake dhidi ya uchokozi wa Urusi.”

Soma pia:Urusi: NATO yaandaa mazingira ya Vita vya Tatu vya Dunia

Ujerumani, ambayo ilikuwa imekabiliwa na mbinyo baada ya kukataa maombi ya Ukraine ya kupeleka silaha nzito, imetangaza kuwa itapeleka vifaru vya kupambana na mashambulizi ya ndege za kijeshi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza mjini Moscow jana, alitoa pendekezo la jinsi ya kuwahamisha watu kutoka mji wa Ukraine uliozingirwa wa Mariupol, likihusisha Kundi la Mawasiliano ya Kiutu la Urusi, Ukraine na maafisa wa Umoja wa Mataifa. Ukraine ilisema hakuna maeneo salama yaliyofunguliwa jana kutokana na mapigano yanayoendelea.

Russland | Treffen UN-Generalsekretär Antonio Guterres und Wladimir Putin in Moskau
Putin na Guterres walijadili hali ya kiutu MariupolPicha: Vladimir Astapkovich/AP/Sputnik/Pool/dpa/picture alliance

Umoja wa Mataifa umesema Rais Vladmir Putin alikubali kimsingi wakati wa mazungumzo yake na Guterres kuhusu ushiriki wa Umoja wa Mataifa na Msalaba Mwekundu katika kuwahamisha raia kutoka kiwanda cha chuma cha Azovstal mjini Mariupol, eneo ambalo limeshuhudia mapigano makali zaidi katika vita hivyo.

Nguvu za kura ya turufu

Kwingineko, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepiga hatua ya kwanza ya kuziweka nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama chini ya kurunzi wakati wanapotumia nguvu yao ya turufu. Hii inatokana na kura ya turufu ya Urusi na kitisho cha kura za turufu katika siku za usoni ambacho kimezuia kuchukuliwa hatua yoyote na taasisi hiyo yenye nguvu ya Umoja wa Mataifa kuhusu vita vya Ukraine.

Soma pia: Umoja wa Mataifa wahitaji dola bilioni 2.2 za msaada Ukraine

Azimio hilo ambalo liliidhinishwa kwa makubaliano na baraza hilo lenye nchi 193 wanachama, haliondoi au kupunguza nguvu ya turufu ya wanachama wa kudumu ambao ni Marekani, Urusi, China, Uingereza na Ufaransa.

Lakini kwa mara ya kwanza, italihitaji Baraza Kuu kufanya mjadala kuhusu hali itakayosababisha kutumiwa kwa kura ya turufu katika Baraza la Usalama katika siku kumi za kazi, na kuwahitaji wanaotumia kura yao ya turufu kueleza ni kwa nini wanaitumia.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/AFP/DPA/AP