1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pigo kwa vyama baada ya wagombea kuenguliwa Zanzibar

Admin.WagnerD21 Septemba 2020

Wakati kampeni zikipamba moto baadhi ya vyama vimepata pigo baada ya wagombea wao kuenguliwa katika kinyanganyiro cha Ubunge, Uwakilishi na Udiwani kutokana na kudaiwa kwenda kinyume na sheria za uchaguzi.

https://p.dw.com/p/3incg
Seif Sharif Hamad
Picha: DW/S. Khamis

Wakati kampeni zikipamba moto kuelekea uchaguzi mkuu mwezi ujao baadhi ya vyama vimepata pigo baada ya wagombea wao kuenguliwa katika kinyanganyiro cha Ubunge, Uwakilishi na Udiwani kutokana na kudaiwa kwenda kinyume na sheria za uchaguzi, huku mikutano ya kampeni ya vyama mbali mbali ikiendelea kwa vyama vyenye ushindani mkubwa wakipishana katika kunadi sera za vyama vyao na vyama vyengine visivyo na ushawishi mkubwa navyo vikijitahidi katika kusaka uungwaji mkono na wapiga kura wa maeneo tofauti. 

Chama chenye ushindani kwa CCM kwa upande wa Zanzibar ni ACT Wazalendo ambacho kimepoteza wawakilishi 13, wabunge 7, na madiwani sita ambao wameenguliwa katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu.

Mkurugenzi wa uchaguzi, tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) Thabit Idarous Faina amesema kuenguliwa kwa wagombea hao ina maana hawaruhusiwi kuendelea na harakati za uchaguzi baada ya rufaa zao kutupiliwa mbali ambapo tume ya uchaguzi ndio muamuzi wa mwisho, na hapa anaeleza.

Tansania Sansibar | Queen Cuthbert Sendiga, Wahlkampf
Mgombea wa chama cha ADC Queen Cuthbert Sendiga akinadi sera zake Visiwani Zanzibar Picha: DW/S. Said

Vyama vyenye ushindani mkubwa hapa Zanzibar vya CCM na ACT Wazalendo vinapishana katika kunadi sera zao ilipoondosha mguu wake CCM ndipo ilipoweka mguu wake ACT Wazalendo huko Nungwi Mkoa wa kaskazini Unguja.

Vyama vyengine vya NRA, DP, CUF, Chauma na UPDP vikinadi sera zao vimeahidi kupambana na rushwa kukabiliana na tatizo la udhalilishaji na kutoa kipaumbele kwa wanawake na kushughulikia kero za muungano.

Miongoni mwa ahadi zilizotolewa na Mgombea Urais wa Zanzibar wa DP Shafi Hassan Suleiman ni kuimarisha uchumi wa viwanda na kupunguza ajira kwa vijana.

Pamoja na kampeni hizo kuendelea lakini hamasa ya wananchi na mashabiki wa siasa wanaonekana kupungua mikutanoni kusikiliza sera za vyama hivyo ambapo wachunguzi wanahusisha hali hiyo na ugumu wa maisha pamoja na kukata tamaa ya kutokuwepo kwa uhuru na demokrasia.

Salma Said- Zanzibar