1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pelosi awasili Taipei licha ya vitisho vya China

Saleh Mwanamilongo
2 Agosti 2022

Awali China ilitahadharisha kuwa Marekani italipa gharama ikiwa Spika wa Bunge Nancy Pelosi atazuru Taiwan. Wakati huo huo Urusi imesema imefungamana na China, na kuita matarajio ya ziara ya Pelosi kuwa uchokozi mtupu.

https://p.dw.com/p/4F1qK
Taiwan I Asien I Nancy Pelosi
Picha: Chiang Ying-ying/AP/picture alliance

Matarajio ya Pelosi kwenda Taipei, ambayo itakuwa ziara ya hadhi ya juu zaidi ya afisa aliyechaguliwa wa Marekani katika miaka 25, imesababisha tahadhari kali kutoka Beijing ambayo imeliweka eneo hilo katika hali ya utata.

Pelosi,mwenye umri wa miaka 82, bado hajathibitisha rasmi kama Taiwan ni sehemu ya ziara inayoendelea Asia lakini vyombo vya habari vya Marekani na Taiwan vimeripoti kuwa itafanyika.

Soma pia→Ziara ya Pelosi Asia wagubikwa na usiri ikiwa atazuru Taiwan

Hatua zozote zinazochukuliwa na china ni za haki

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Hua Chunying amesema katika mkutano wa kawaida na waandishi habari kwamba upande wa Marekani utabeba dhamana na kulipa gharama ya kudhoofisha maslahi ya usalama ya China.

''Marekani na Taiwan zimeshirikiana kufanya chokochoko kwanza, na China imelazimika tu kujilinda. Mbele ya tabia mbaya ya Marekani ya kudharau malalamiko ya mara kwa mara na makubwa ya China, hatua zozote zinazochukuliwa na China zitafahamika kuwa za haki na lazima. Pia ni haki ya mataifa yote huru",alisema Chunying.

Urusi yaingua mkono China

Wandishi habari wakisubiri kuwasili kwa Nancy Pelosi kwenye uwanja wa ndege wa Taipei, nchini Taiwan
Wandishi habari wakisubiri kuwasili kwa Nancy Pelosi kwenye uwanja wa ndege wa Taipei, nchini TaiwanPicha: DW Chinese

China inaichukulia Taiwan inayojitawala na ya kidemokrasia kuwa eneo lake na imeapa siku moja kukiteka kisiwa hicho kwa nguvu ikibidi. Kwenye mazungumzo ya simu na Rais wa Marekani Joe Biden wiki iliyopita, Rais wa China Xi Jinping aliionya Marekani dhidi ya kile alichokiita kucheza na moto juu ya Taiwan.

Wakati huo huo, Urusi imesema imefungamana pamoja na China, ikiita matarajio ya ziara ya Pelosi kuwa uchokozi mtupu. China imekataa kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na imeshutumiwa kwa kutoa hifadhi ya kidiplomasia kwa Ikulu ya Kremlin kwa kukiuka vikwazo vya nchi za Magharibi na kuzuia uzwaji wa silaha kwa Ukraine.

Soma pia→China yaishutumu Marekani kwa kuipaka tope

Mashambulio ya mtandaoni?

Leo Jumanne, ofisi ya rais wa Taiwan ilisema tovuti yake ilivamiwa kwa muda wa dakika 20 kufuatia shambulio la mtandaoni. Haikuwa wazi kwa nini, lakini ofisi ilisema itachunguza kile ilichoelezea kuwa ni jaribio kutoka nje. Jeshi la kisiwa hicho mnamo Jumanne lilisema limedhamiria kukilinda dhidi ya vitisho vilivyoongezeka kutoka kwa China kufuatia uwezekano wa ziara ya Pelosi.

Watu milioni 23 wa kisiwa hicho wameishi kwa muda mrefu na uwezekano wa uvamizi, lakini tishio hilo limeongezeka chini ya Xi Jinping, kiongozi wa China mwenye uthubutu zaidi.