1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pelosi alaani mashambulizi ya Azerbaijan dhidi ya Armenia

(Tafsiri: John Juma)19 Septemba 2022

Spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi amelaani 'shambulizi ambalo ni kinyume cha sheria' ambalo limefanywa na Azerbaijan dhidi ya Armenia na kuzusha mapigano mabaya zaidi tangu kuanza kwa vita hivyo mwaka 2020.

https://p.dw.com/p/4H38c
Armenien | Nancy Pelosi besucht Jerevan
Picha: KAREN MINASYAN/AFP/Getty Images

Hayo yakijiri Urusi imetoa tamko kuhusu kauli na ziara ya Pelosi ikisema nchini Armenia ikisema ziara ya kimya na kutumia mbinu za kibiashara ni bora zaidi katika kuleta utulivu, kuliko kutangaza maneno kwa sauti ya juu.

Azerbaijan na Armenia zimekuwa zikilaumiana kuhusu nani alianzisha machafuko katika mpaka kati yao Jumanne wiki iliyopita, ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 200.

Armenia na Azerbaijan zakubaliana kusitisha mapigano

Akizungumza na waandishi wa habari Yerevan, mji mkuu wa Armenia, spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi amesema kwa niaba ya bunge la nchi yake, anayalaani mashambulizi hayo yanayotishia matarajio ya makubaliano ya amani yanayohitajika.

"Usalama na uhuru wa Armenia, demokrasia ya Armenia ni ya thamani kwetu Marekani. Na uhusiano wetu na nchi nyingine kwenye mgogoro huu, tunapaswa kutumia ushawishi na uwezo wetu kuonesha kwamba demokrasia ya Armenia na uhuru wake ni kipaumbele,” amesema Pelosi.

Mkuu wa Baraza la Usalama la Armenia Artyom Grigoryan alisema waliwasilisha ombi la msaada wa kijeshi kwa Urusi, ila ombi lao halikukubaliwa, na hawajafurahishwa na hilo.
Mkuu wa Baraza la Usalama la Armenia Artyom Grigoryan alisema waliwasilisha ombi la msaada wa kijeshi kwa Urusi, ila ombi lao halikukubaliwa, na hawajafurahishwa na hilo.Picha: Dimitar Dilkoff/AFP/Getty Images

Spika wa bunge la Armenia Alen Simonyan alisema uhasama kati ya pande hizo mbili ulimalizika usiku wa kuamkia Ijumaa, kufuatia upatanishi ulioongozwa na Marekani. Akiwa na Nancy Pelosi, Simonyan aliwaambia waandishi wa habari kwamba wanaishukuru Marekani kwa kuwezesha makubaliano hayo ya kusitisha mapigano. Juhudi za awali za Urusi kumaliza mapigano hayo zilifeli.

Je ushawishi wa Urusi katika mzozo wa Armenia na Azerbaijan unafifia?

Urusi ambayo hapo awali pia ilishutumu mara kadhaa ziara ya Pelosi kule Taiwan, inatizama nchi za Armenia na Azerbaijan kama kanda yake ya kudhihirisha ushawishi wake na hivyo inatizama hatua za Marekani kama kuingilia masuala ya kanda hiyo.

Urusi tayari ipo kwenye mkataba unaoipa jukumu la kuilinda Armenia endapo itavamiwa kutoka nje, lakini ambayo pia ina ukaribu na Azerbaijan, haikuisaidia Yerevan mapema licha ya ombi rasmi la kutaka msaada wa kijeshi.

Mapigano yazuka upya mpaka wa Armenia na Azerbaijan

Mkuu wa Baraza la Usalama la Armenia Artyom Grigoryan alisema waliwasilisha ombi la msaada wa kijeshi, ila ombi lao halikukubaliwa, na hawajafurahishwa na hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, pia alizungumza na rais wa Azerbaijan Llham Aliyev siku ya Jumapili kwa njia ya simu.

Blinken ataka masuala tete yaliyosalia yatatuliwe kwa mazungumzo

Kulingana na msemaji wa wizara hiyo Ned Price, Blinken alimhimiza Rais Aliyev kuzingatia makubaliano ya usitishaji vita na aviondoe vikosi vyake kijeshi eneo hilo na afanyie kazi masuala yote ya yaliyosalia yenye utata kati ya Armenia na Azerbaijan kwa njia ya mazungumzo ya amani.

Ziara ya spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi nchini Armenia inaashiria kuongezeka kwa ukaribu au uhusiano kati ya Washington na Yerevan. Mafadhaiko ya Armenia yamekuwa yakiongezeka kufuatia kutoungwa mkono na mshirika wake wa zamani Urusi ambayo imekengeushwa na vita vya Ukraine ambavyo vimedumu kwa takriban miezi saba sasa.

Pelosi aliyewasili Yerevan Armenia siku ya Jumamosi kwa ziara ya siku tatu, ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi wa Marekani kuwahi kuitembelea nchi hiyo ndogo tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka uliokuwa muungano wa Sovieti mwaka 1991.    

(Afpe, Rtre)