1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pazia la kampeni lafungwa nchini Uganda

12 Januari 2021

Muda wa kampeni za uchaguzi nchini Uganda umemalizika na kinachosubiriwa sasa ni zoezi la uchaguzi litakalofanyika  siku ya Alhamisi. Lakini taharuki inazidi kufuatia matumizi ya mitandao na majukwaa ya kijamii kuwa yenye matatizo huku askari polisi na majeshi wakionekana kuongezeka katika mitaa na barabara za miji.

https://p.dw.com/p/3npbe

Kisheria, saa kumi na mbili kamili za jioni ndiyo wakati kampeni za uchaguzi zimekamilika.

Kampeni za urais zimechukua siku sitini na katika muda huo, kumekuwepo na visa kadhaa vya ghasia na makabiliano kati ya wafuasi wa upinzani na askari majeshi na polisi.

Hali hii ndiyo inahofiwa siku ya uchaguzi na zile zitakazofuata wakati matokeo yakitangazwa hasa watu wakihisi kwamba udanganyifu umefanyika.

Ni kwa msingi huu ndipo Waziri mkuu wa ufalme wa Buganda amehimiza tume ya uchaguzi kufahamu kuwa inabeba dhamana ya nchi na ifanye kazi yake ipasavyo ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki.

Uganda Kampala | Porträt von Robert Kyagulanyi, Präsidentschaftskandidat
Bango la kampeni la mgombea urais wa upinzani Bobi Wine Picha: Lubega Emmanuel/DW

Lakini taarifa za wafuasi wa chama cha NUP walio na uhusiano wa karibu na mgombea urais Robert Kyagulanyi maarufu yaani Bobi Wine kushambuliwa asubuhi ya leo na baadhi kukamatwa ni vitendo ambavyo vinaelezewa kuleta hofu na wasiwasi miongoni mwa wapiga kura. 

Polisi yamtuhumu Bobi Wine kutaka kujiteka 

Ijapokuwa hakugusia suala hilo, msemaji wa polisi Fred Enanga amedai kuwa wana taarifa kuwa mgombea huyo amepanga njama kutoweka mara tu baada ya kupiga kura na kujificha katika ubalozi mmoja ambao hakuutaja.

Ameongeza kuwa Bobi Wine anadhani hali hii itasababisha wafuasi wake kuzusha ghasia wakiita serikali ifahamishe kuhusu mahali aliko.

Wafuasi wa Bobi Wine wamesema huo ni uzushi tu ili vyombo vya usalama vipate kisingizio cha kumweka mgombea huyo katika kizuizi cha nyumbani.

Kwingineko, matumizi ya mitandao ya kijamii na intaneti kwa jumla imekuwa ya shida kwa watumiaji nchini Uganda siku ya leo.

Uganda Präsident Yoweri Museveni
Rais Yoweri Museveni wa Uganda anawania muhula mwingine madarakani Picha: Reuters/J. Akena

Mamlaka ya mawasiliano imekanusha madai kwamba ndiyo inasababisha hali hii ambayo inahofiwa hapo baadaye huduma hizo zitafungiwa kabisa.

Kwa upande wake msemaji wa serikali Ofwono Opondo amesema hajali kama huduma hizo hazipo maana kampuni ya Facebook imeonyesha waziwazi kwamba inalenga kuvunja mawasiliano ya chama tawala cha NRM kuwafikia wafuasi wake.

Wakati huohuo, rais Museveni ametangaza orodha mpya ya wakuu wa wilaya na manaibu wao.

Maafisa hao ni wawakilishi wa utawala mashinani na mageuzi hayo kufanyika wakati huu imewashangaza wengi lakini ikikumbukwa kuwa alitamka kuwa ana taarifa kwamba baadhi yao walikuwa wana njama za kushiriki wizi wa kura kupendelea upinzani.