1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PARIS: Maandamano yaendelea mjini Paris, Ufaransa

3 Novemba 2005
https://p.dw.com/p/CEMG

Maandamano yameendelea kwa usiku wa saba katika viunga vya mji wa Paris nchini Ufaransa. Polisi wa kuzima fujo wamelengwa kwa risasi na waandamanaji katika kitongoji cha La Courneuve usiku wa kuamkia hii leo, lakini hakuna ripoti za majeruhi zilizotolewa.

Duru za polisi zinasema makundi ya vijana wamechoma magari, kuvunja maduka na kuharibu shule mbili za msingi. Vijana hao wameapa kuendelea kupambana na polisi mpaka polisi watakapokoma kuwachokoza katika makaazi yao wakati wa usiku. Maofisa wa serikali wanaonekana wameshindwa kuzuia wimbi la machafuko ambalo limekuwa likiendelea kwa juma moja kuenea katika maeneo mbalimbali.

Waziri mkuu wa nchi hiyo, Dominique de Villepin na waziri wa mambo ya ndani Nicolas Sarkozy wamefutilia mbali ziara zao katika mataifa ya kigeni ili kukabiliana na machafuko hayo.

Machafuko ya Paris yalizuka wiki iliyopita baada ya vijana wawili kuuwawa na umeme wakati walipokuwa wakiwakimbia polisi.