1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaParaguay

Paraguay yaipigia chapuo Taiwan kujiunga Umoja wa Mataifa

20 Septemba 2023

Rais Santiago Pena wa Paraguay amesema nchi yake inaunga mkono dhamira ya kisiwa cha Taiwan ya kujiunga na Umoja wa Mataifa na mashirika yake.

https://p.dw.com/p/4WZxQ
Rais Santiago Pena wa Paraguay (kushoto) na rais Tsai Ing-wen wa Taiwan
Rais Santiago Pena ni mshirika mkubwa wa Taiwan. Pichani akikutana na rais Tsai Ing-wen wa Taiwan mnamo Julai 12, 2023 alipoitembelea Taipei.Picha: Taiwan Presidential Office/Reuters

Pena ametoa matashi hayo katika hotuba yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa aliyoitoa usiku wa kuamkia leo.

Kiongozi huyo wa Paraguay, taifa pekee la Amerika ya Kusini ambalo bado linaitambua Taiwan kuwa nchi kamili, amesema ni muhimu kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kulitafutia jawabu suala la hadhi ya Taiwan.

Kisiwa hicho chenye utawala wake wa ndani kilizuiwa kuchukua kiti kwenye Umoja wa Mataifa na mashirika yake mwaka 1971 baada ya chombo hicho kuitambua Jamhuri ya Umma wa China kuwa mwakilishi rasmi wa China ndani ya umoja huo.

China inaizingatia Taiwan kuwa sehemu ya milki yake licha ya kisiwa hicho kuipinga vikali sera hiyo.