1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiItaly

Papa Francis: Wakumbukeni wanyonge na maskini

25 Desemba 2022

Papa Francis amesema vita na machafuko mengine kutokana na uchoyo na tamaa ya madaraka vimesababisha wengine hata kuwaangamiza majirani zao.

https://p.dw.com/p/4LPZZ
Vatikan Christmette Papst Franziskus
Picha: Andreas Solaro/AFP/Getty Images

Kwenye hotuba yake iliyoonekana kulenga vita vya Ukraine, Papa Francis amesema vita na machafuko mengine kutokana na uroho na tamaa ya madaraka vimesababisha wengine hata kuwaangamiza majirani zao.

Akisherehekea Krismasi ya 10 ya upapa wake, Francis aliongoza maombi ya mkesha wa Krismasi katika kanisa la Mtakatifu Petero na kuhudhuriwa na takriban waumini 7,000.

Hii ilikuwa mara ya kwanza katika miaka miwili tangu janga la COVID kuanza, kwa umati mkubwa wa waumini kuhudhuria misa hiyo ya mkesha wa Krismasi mjini Rome.

Takriban waumini wengine 4,000 walifuatilia misa hiyo wakiwa nje kwenye viwanja vya kanisa hilo. Hotuba ya Papa Francis ilijikita katika mada ya uchoyo na matumizi katika viwango tofautitofauti.

Aliwataka waumini kutafakari zaidi kuhusu matumizi makubwa ambayo hushuhudiwa kwenye sherehe za Krismasi.

Badala yake wabaini maana halisi ya Krismasi ili wawakumbuke wale wanaoteseka kutokana na vita na umaskini.

"Wanaume na wanawake katika ulimwengu wetu, katika njaa yao ya kutaka utajiri na madaraka, wanawaangamiza hata majirani, kaka na dada zao," alisema. "Ni vita vingapi tumeona! Na katika maeneo mangapi, hata leo, je utu na uhuru wa binadamu zinadharauliwa?"

Papa Francis amekuwa akikemea vita vya Ukraine

Gari lililoharibiwa mjini Kherson kufuatia mashambulizi ya vikosi vya Urusi nchini Ukraine Disemba 24, 2022.
Gari lililoharibiwa mjini Kherson kufuatia mashambulizi ya vikosi vya Urusi nchini Ukraine Disemba 24, 2022.Picha: Igor Burdyga/DW

Tangu Urusi ilipoivamia jirani yake Ukraine Februari 24, Papa Francis amevikemea vita hivyo karibu katika kila hafla yake ya hadharani, angalau mara mbili kila wiki, huku akilaani kile anachokiita kuwa ukatili na uchokozi usiokuwa na msingi.

Hata hivyo katika hotuba yake ya usiku wa kuamkia Jumapili, Papa Francis hakuitaja Ukraine.

"Kama ilivyo kawaida, waathiriwa wa uchoyo huu wa kibinadamu ni wanyonge wasiojiweza na walioko hatarini," alisema hayo huku akishutumu ulimwengu uliojaa tamaa ya fedha, madaraka na anasa…"

"Zaidi ya yote, ninawafikiri watoto ambao wameuliwa kutokana na vita, umaskini na dhuluma," akiwataja pia watoto ambao hawajazaliwa, watu maskini na watoto waliosahaulika.

Akilinganisha hali ya Yesu Kristo aliyezaliwa horini mwa ng'ombe na umaskini wa leo, Papa alisema: "Horini penye hali ngumu na kukataliwa Mungu alijitokeza mwenyewe. Anakuja hapo kwa sababu tunaweza kuona shida ya ubinadamu wetu: Hali hiyo ya kutokujali na ukosefu wa usawa unasababishwa na uchoyo wa kumiliki vitu na kuvitumia.

Mapema mwezi huu, Francis aliwahimiza watu kupunguza matumizi yao kwenye sherehe za Krismasi na zawadi. Badala yake watume fedha watakazobaki nazo kwa Waukraine ili kuwasaidia wakati huu wa majira ya baridi kali.

Anatarajiwa kutoa hotuba nyingine leo ya siku yenyewe ya kusherehekea Krismasi kwa wakaazi wa Roma na ulimwengu kwa jumla katika kanisa hilo la Mtakatifu Petero (St. Peter's Basilica).

Chanzo: Reuters