Papa Francis kuendeleza ujumbe wa amani Sudan Kusini
3 Februari 2023Ziara hii inayoitwa iliyopewa jina la "Hija ya amani" ni ziara ya kwanza kabisa ya Papa Francis nchini Sudan Kusini tangu taifa hilo lenye Wakristo wengi kupata uhuru kutoka kwa Sudan yenye Waislamu wengi mwaka 2011 baada ya miongo kadhaa ya migogoro.
Hii inafuatia ziara ya siku nne nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo mzozo wa kikatili unaeoendelea kufukuta katika eneo la mashariki lenye utajiri wa madini ulikuwa muhimu katika ajenda ya Kiongozi hiyo.
Amani ilitoweka pia Sudan Kusini, ambako vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano vimesababisha vifo vya watu wapatao 380,000 huku wengine milioni nne wakilazimika kuyahama makazi yao, na kuiacha nchi hiyo changa katika umaskini mkubwa.
Umati wa watu ulikusanyika katika mitaa ya Juba saa chache kabla ya Papa Francis kuwasili, wakipeperusha bendera ya taifa na kushikilia mabango ya kumkaribisha nchini Sudan Kusini. Baadhi ya watu walivaa mavazi ya kitamaduni na kidini, huku wengine wakipiga baragumu, miluzi, na kuimba nyimbo mbalimbali.
Ziara ya amani
Papa huyo mwenye umri wa miaka 86 anatarajiwa kukutana na waathiriwa wa migogoro, pamoja na viongozi wa kisiasa na makanisa nchini humo, lakini pia anatarajiwa kuongoza shughuli za maombi na misa ambayo inatarajiwa kuwavuta umati mkubwa wa watu.
Soma zaidi: Papa Francis kuelekea Sudan Kusini baada ya Congo
Ziara hiyo ya tano ya Papa Francis barani Afrika ilipangwa kufanyika mnamo 2022 lakini iliahirishwa kutokana na tatizo la goti la kiongozi huyo. Adha hiyo imemfanya ategemee matumizi ya kiti cha magurudumu huku muda wa ziara yake ukipunguzwa katika nchi zote mbili alizozitembelea wakati huu.
Papa Francis ataungana huko Sudan Kusini na Askofu Mkuu wa Canterbury pamoja na Msimamizi wa Mkutano Mkuu wa Kanisa la Scotland, wakisisitiza wito mpana wa Ukristo katika nchi hiyo iliyo na jumla ya waumini milioni 12.
Soma zaidi: Papa Francis awarai vijana wa Kongo kupiga vita rushwa
Papa Francis aliahidi mwaka 2019 kusafiri hadi Sudan Kusini alipowakaribisha huko Vatican viongozi wawili hasimu wa nchi hiyo ambao ni Rais Salva Kiir na naibu wake Riek Machar, na kuwataka kuheshimu usitishaji vita.
Papa Francis aliwashangaza wengi kwa kupiga magoti na kuibusu miguu ya mahasimu hao wawili ambao majeshi yao yalishutumiwa kwa uhalifu wa kivita. Lakini miaka minne baadaye, nchi hiyo imesalia katika mzozo usioelezeka.