1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiVatican

Papa Francis amtembelea papa mstaafu Benedict anayeumwa

28 Desemba 2022

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amemtembelea mtangulizi wake papa mstaafu Benedict wa XVI, baada ya afya yake kudhoofika katika saa chache zilizopita.

https://p.dw.com/p/4LV8S
Ehem. Papst Benedikt XVI
Picha: Stefano Spaziani/picture alliance

Mapema Jumatano, Papa Francis alitangaza kuwa afya ya papa wa zamani, mwenye umri wa miaka 95 imedhoofika na kuwaomba waumini wamuombee ili Mwenyezi Mungu aweze kumjalia uponyaji wake na kumfariji.

''Napenda kuwaomba nyote msali sala maalum kwa ajili ya kumuombea Papa mstaafu Benedict, ambaye kwa ukimya analitegemeza Kanisa. Tumkumbuke. Ni mgonjwa sana, tunamuomba Mungu amfariji na kumtegemeza katika ushuhuda huu wa upendo kwa Kanisa hadi mwisho,'' alifafanua Papa Francis.

Benedict aliumwa kabla ya Sikukuu ya Krismasi

Aidha, msemaji wa Vatican Matteo Bruni, amesema hali ya Benedict wa XVI imedhoofika kutokana na umri wake mkubwa bila ya kutoa maelezo zaidi. Bruni amesema Benedict yuko chini ya uangalizi wa madaktari na afya yake iko imara. Nalo shirika la habari la Italia, ANSA, limeeleza kuwa afya ya Benedict ilianza kudhoofika kabla ya Sikukuu ya Krismasi, baada ya kusumbuliwa na matatizo ya kupumua.

Askofu Mkuu, Georg Gaenswein, msaidizi binafsi wa Benedict, hakupatikana mara moja kuzunguzia suala hilo. Askofu huyo amekuwa akimsaidia Benedict kwa miaka kadhaa katika makaazi yake kwenye Monasteri ya Mama wa kanisa huko Vatican, anakoishi tangu alipostaafu mwaka 2013.

Vatikan | Papst Franziskus
Papa Francis akizungumza na waumini katika ukumbi wa Paul V1, VaticanPicha: FILIPPO MONTEFORTE/AFP

Benedict, mzaliwa katika jimbo la Bavaria nchini Ujerumani, ambaye jina lake halisi ni Joseph Aloisius Ratzinger, alichaguliwa kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Aprili 19, 2005, baada ya kifo cha mtangulizi wake John Paul wa II.

Nchini Ujerumani, mkuu wa baraza la maaskofu Katoliki, Askofu Georg Baetzing, ameungana na Papa Francis kutoa wito kwa waumini kumuombea papa mstaafu. Akizungumza na shirika la habari la Ujerumani, DPA askofu huyo wa Limburg amesema anamuombea Benedict uponyaji wa haraka.

Scholz aungana na Papa Francis kumuombea Benedict

Askofu Mkuu wa Munich na Freising, Mhashamu Rheinhard Marx amesema anaungana na Papa Francis kumuombea Benedict, na hivyo leo atajumuika na hasa vijana Wakristo kumuombea.

Mjini Berlin, Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amemtakia papa mstaafu ahueni njema akisema wako pamoja naye wakati huu. Hayo yameelezwa Jumatano na msemaji wa serikali, Christiane Hoffmann katika mkutano wa kawaida na waandishi habari.

Benedict, ambaye Februari 28, mwaka 2013 alikuwa papa wa kwanza kujiuzulu katika kipindi cha miaka 600 iliyopita, afya yake imekuwa ikidhoofika katika miaka ya hivi karibuni, na amekuwa akiendelea kujitolea katika maisha yake baada ya kuwa papa kwa kuomba na kutafakari.

(DPA, AP, AFP)