1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis aanza rasmi ziara yake katika Falme za Kiarabu

4 Februari 2019

Ziara hiyo ya kiongozi wa kanisa Katoliki duniani ni ya kwanza kuwahi kufanywa na kiongozi wa kanisa hilo kwenye rasi ya Uarabuni. Lengo ni kufungua ukurasa mpya katika uhusiano baina ya wakristo na Waislamu.

https://p.dw.com/p/3CfjH
Vereinigte Arabische Emirate Papst in Abu Dhabi gelandet
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Medichini

Mrithi wa mfalme wa Abu Dhabi Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan alimlaki Papa Francis kwenye  uwanja wa ndege akiwa na tabasamu huku akiongozana na mawaziri wake. Imam mkuu wa msikiti maarufu  wa Al-Azhar wa nchini Misri, Ahmed el Tayeba pia alikuwapo uwanja wa ndege kumlaki Baba Mtakatifu. Leo hii Papa Francis na imam el Tayeb watahutubia kwenye mkutano utakaohudhuriwa na wawakilishi wa dini zote. Hapo kesho Papa Francis ataongoza misa itakayokuwa ya kwanza kuongozwa na baba mtakatifu kwenye rasi ya Uarabuni. Waumini wapatao 135,000 wanatarajiwa kuhudhuria misa hiyo ya hadharani.

Baadae leo mgeni huyo kutoka Vatican atautembelea msikiti mkuu na pia atakutana kwa faragha na wazee wa baraza la Waislamu. Papa Francis pia atahudhuria mdahalo wa kimataifa wa dini zote utakaofanyika  katikati ya mji wa Abu Dhabi.

Juu ya ziara ya Papa Francis kwenye rasi ya Uarabuni mkurugenzi mtendaji wa asasi ya kupambana na itikadi kali Maqsoud Kruse amesema jambo mahsusi juu ya ziara hiyo ni kwamba inafungua njia ya hatua muhimu kabisa ya mdahalo kati ya tamaduni mbalimbali na muhimu ni kwamba stahamala inafuatiwa pamoja na hatua thabiti.

Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis
Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa FrancisPicha: Getty Images/AFP/T. Fabi

Kabla ya kuwasili Uarabuni baba  mtakatifu alitoa mwito kwa pande zote zinazohusika na mgogoro wa nchini Yemen wa kutekeleza makubaliano ya kusimamisha vita ili mahitaji ya chakula na dawa yaweze kuwafikia watu  wanaokabiliwa na mgogoro mkubwa wa  kibinadamu usiokuwa na kifani duniani.

Umoja wa Falme za Kiarabu ni mshirika mkuu wa Saudi Arabia katika vita vya nchini Yemen. Hatua ya baba mtakatifu kutoa wito huo kabla ya kuanza ziara ni kuepusha kuwaumbua wenyeji wake. Kiongozi huyo wa kanisa Katoliki amesema Mungu anasikia vilio vya watoto wanaotaabika chini ya mazingira ya kivita.

Hata hivyo Papa Francis anafanya ziara kwenye rasi ya Uarabuni wakati ambapo pana mivutano katika ukanda huo. Misiri, Bahrain, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za nchi za kiarabu zimeisusia Qatar tangu  mwaka 2017.

Mwandishi:Zainab Aziz/AP/DPAE

Mhariri:  Iddi Ssessanga