Palestina yaahirisha uchaguzi wa Bunge
30 Aprili 2021Abbas ametoa tangazo hilo baada ya mkutano na wawakilishi wa makundi kadhaa ya wapalestina mjini Ramallah na kusema uchaguzi huo hautafanyika hadi serikali yake itakapopata hakikisho kuwa eneo la Jerusalem Mashariki pia litashiriki kupiga kura.
Haijafahamika iwapo uchaguzi wa rais uliopangwa mnamo mwezi Julai ambao utakuwa wa kwanza tangu mwaka 2005 utaendelea au nao pia umeahirishwa.
Duru kutoka Palestina zinasema uamuzi huo unatokana na Israel kushindwa kuridhia matakwa ya mamlaka za Palestina za kuruhusu upigaji kura kufanyika pia kwenye eneo hilo la mji wa Jerusalem ambalo linakaliwa kwa mabavu.
Abbas ailaumu Israel kwa mkwamo uliotokea
Kupitia hotuba yake kwa watu wa Palestina, Abbas ameilaumu Israel kwa kushindwa kuweka wazi iwapo itaruhusu uchaguzi huo wa bunge ufanyike mjini Jerusalem kama ilivyopangwa kwa eneo la Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.
Abbas ameutaja mvutano kuhusu ushiriki wa Jerusalem kuwa sababu kuu ya uamuzi wa kuahirisha uchaguzi ambao ungekuwa wa kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 15.
"Tumepiga hatua kubwa na Jumuiya ya Kimataifa ya kutaka nchi inayotukalia kwa mabavu ilazimishwe kutoa ahadi kuhusu Jerusalem, lakini hadi sasa majaribio yote hayo yamekabiliwa na vizingiti. Iwapo wataridhia hata ndani ya saa moja, hatutasita kufanya uchaguzi" amesema Abbas.
Israel imekwishasema kwamba bado hakuna tangazo rasmi juu ya iwapo itaruhusu kufanyika kwa uchaguzi mjini Jerusalem kama ilivyofanya wakati wa uchaguzi wa mwaka 2006.
Wakati wa uchaguzi wa mwisho, wakaazi wa Jerusalem Mashariki walipiga kura kwenye maeneo ya pembezoni mwa mji na maelfu wengine kwenye ofisi za posta baada ya Israel kuridhia zoezi hilo kufanyika.
Uamuzi huo utachochea misuguano ndani ya Palestina
Uamuzi wa kuahirisha uchaguzi umekuja miezi mitatu tangu Abbas alipoutangaza katika kile kilichoonekana kuwa jibu kwa ukosoaji unaondama uhalali wa kidemokrasia wa taasisi za mamlaka ya Palestina ikiwemo wadhifa wake wa urais.
Kucheleweshwa kwa uchaguzi huo kunaweza kuzidisha ukosoaji wa ndani kwa Abbas na washirika wake wa chama cha Fatah ambao kura za maoni ya umma tayari zinaonesha kuwa wanapoteza uungwaji mkono.
Kundi la Hamas ambalo linatawala ukanda wa Gaza ulio sehemu ya mamlaka ya ndani ya Palestina limekwishasema kuwa halikubaliani na uamuzi wa kuahirishwa kwa uchaguzi.Uchaguzi huo wa bunge ulikuwa sehemu ya juhudi za kuleta maridhiano kati ya kundi la Hamas na chama cha Fatah ambayo yangefanikisha kufikiwa makubaliano ya kuanzishwa mazungumzo mapya na Israel kuhusu suluhisho la kuundwa madola mawili kama njia ya kumaliza mzozo kati ya Israel na Palestina.