1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan kuwaadhibu vikali wabakaji

16 Desemba 2020

Rais wa Pakistan amepitisha sheria mpya ya kushughulikia haraka unyanyasaji wa kijinsia baada ya genge la wanaume kumbaka mwanamke mbele ya watoto wake kando ya barabara ambayo haitumika karibu na Lahore.

https://p.dw.com/p/3mmwK
Pakistan Lahore | Protest für Gerechtigkeit nach Vergewaltigung
Picha: DW/T. Shahzad

Pakistan imepitisha sheria mpya ya ubakaji itakayoruhusu kuanzishwa mahalama maalumu za kushughulikia visa vya ubakaji, hii ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuharakisha usikilizwaji wa kesi zinazohusiana na unyanyasaji wa kingoni kwa wanawake na watoto.

Sheria hiyo mpya imechochewa na tukio la ubakaji, baada ya kundi la wanaume kumbaka mwanamke mbele ya watoto wake pembezoni mwa barabara isiyotumika mwezi Septemba. Kundi kubwa la waandamanaji liliandamana nchini humo siku zilizofuata baada ya tukio hilo, wakimshinikiza waziri mkuu Imran Khan kuchukua hatua ya kuzuia uhalifu wa kingono nchini humo.

Sheria hiyo mpya inaanza kutumika mara moja, lakini itahitaji kuridhiwa na bunge katika kipindi cha miezi minne.

Adhabu kali.

"Sheria hiyo itasaidia kushughulikia kesi za unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake na watoto. Mahakama maalumu zitaundwa kote nchini humo kushughulikia kesi hizo na kesi za watuhumiwa wa ubakaji haraka iwezekanavyo" Rais Arif Alvi aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter, jana Jumanne.

Sheria hiyo mpya pia itasaidia uundwaji wa vikosi maalumu dhidi ya ubakaji ambavyo vitafanya uchunguzi wa kitiba katika kipindi cha masaa sita tangu madai yalipowasilishwa kwenye kikosi hicho. Utambulisho wa mhanga unazuiwa chini ya sheria hiyo, lakini itaruhusu usajili wa watuhumiwa wa unyanyasaji huo.

Muswada wa sheria hiyo mpya bado haujachapishwa, lakini waziri wa sheria amesema adhabu ya kifo itakuwa miongoni mwa adhabu kwenye sheria hiyo.

Mashirika: DW