1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ousmane Sonko atoa wito wa maandamano zaidi Senegal

9 Machi 2021

Kiongozi wa upinzani Senegal Ousmane Sonko, ametoa wito wa maandamano makubwa zaidi ya amani baada ya siku kadhaa za vurugu katika taifa hilo la Afrika Magharibi zilizosababishwa na hatua ya kukamatwa kwake

https://p.dw.com/p/3qNtr
Senegal Präsidentschaftswahlen Wahlkampagnen Ousmane Sonko
Picha: DW/R. Ade

Akizungumza mjini Dakar baada ya kuachiliwa huru hapo jana, Ousmane Sonko amesema harakati za kudai mabadiliko zimeanza na hakuna anayeweza kuzizuwia huku akiwahimiza wafuasi wake na raia wa Senegal kwa ujumla kujitokeza kwa wingi na kuandamana lakini akasisitiza maandamano hayo ni lazima yawe ya amani.

Rais wa taifa hilo Macky Sall pia ametoa wito wa amani akiwataka waandamanaji kuachana na vurugu. Sonko ambaye ni mpinzani mkubwa wa rais Sall na mkosoaji wa serikali yake, amekanusha madai ya ubakaji dhidi yake akiyataja kama madai yanayolenga kumchafua kisiasa.

Senegal taifa linalobeba sifa ya kuwa tulivu katika mataifa ya Magharibi limekumbwa na maandamano kuanzia wiki iliyopita baada ya Sonko kukamatwa.

Katika maandamano hayo watu watano waliuwawa akiwemo mwanafunzi mmoja baada ya mapambano kati ya maafisa wa polisi na wafuasi wa upinzani wanaoshikilia msimamo wao kuwa tuhuma dhidi ya kiongozi wao zimenuiwa kumchafulia safari yake ya kiasiasa.

Rais Macy Sall  awataka wasenegal kuwa watulivu

Senegal Präsidentschaftswahlen | Macky Sall
Rais wa Senegal Macky Sall Picha: picture-alliance/Xinhua News Agency/D. Gueye

Hata hivyo Sonko anayeonekana kama mpinzani mkubwa wa rais Macky Sall katika uchaguzi unaokuja wa mwaka 2024, amesema rais huyo hana haki tena ya kuongoza nchi.  Lakini amepinga hatua yoyote ya kumuondoa kwa nguvu madarakani badala yake amesema anasubiri kupambana naye wakati wa uchaguzi.

Rais Macky Sall ameendelea kuwahimiza waandamanaji kuwacha chuki na kutoshiriki matendo yanayosababisha vurugu. Akilihutubia taifa hapo jana Sall amesema mahakama inapaswa kuwachwa kufanya kazi bila kuingiliwa na mtu yeyote.

Maelfu wa wafuasi wa Sonko walimiminika mjini Dakar siku ya Jumatatu baada ya kiongozi wao kushitakiwa kwa tuhuma za ubakaji huku wakiwarushia polisi mawe na kuchoma magari kabla ya maafisa wa polisi kuwatawanya kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi.

Majirani wa taifa hilo la Afrika Magharibi pamoja na Umoja wa Mataifa wameelezea wasiwasi wao juu ya mvutano wa kisiasa na kuhimiza uwepo wa amani. Viongozi wa kidini katika taifa hilo lililo na waislamu wengi na lililo na idadi ya watu milioni 16 pia wametoa wito wa amani.

Chanzo: afp