1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OTAWA-Masingasinga wawili waachiwa huru kutokana na kesi ya uripuaji wa ndege ya abiria ya India mwaka 1985

17 Machi 2005
https://p.dw.com/p/CFWE

Jaji mmoja wa mahakama ya Canada amewaachia huru wanaharakati wawili Masingasinga,kutokana na tuhuma zilizokuwa zikiwakabili za kuripua ndege ya Shirika la Ndege la India katika mwambao wa bahari ya Atlantic nchini Ireland mwaka 1985.Ajali hiyo ya ndege hadi sasa inachukuliwa kuwa ndio ajali mbaya ya ndege ya abiria iliyotokana na kuripuliwa kwa bomu katika historia ya ajali za ndege duniani.

Mashtaka dhidi ya watu hao wawili yalifutwa baada ya jaji kuona kuwa mwendesha mashtaka katika kipindi cha miaka miwili ya usikilizwaji wa kesi hiyo,ameshindwa kuonesha ushahidi unaoweza kuwatia hatiani watuhumiwa hao.

Familia za watu 329 waliokufa katika ajali hiyo ya ndege wameuita uamuzi wa kuachiwa kwa Masingasinga hao kuwa ni kitendo cha kuvunja moyo na wameitaka serikali ya Canada kuunda tume huru itakayochunguza mwenendo wa kesi hiyo.