1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Osama alikuwa nani?

2 Mei 2011

Osama Bin Laden ameuliwa na habari kutangazwa Rais Barack Obama wa Marekani, zikathibitishwa pia na Idara ya Upelelezi ya Pakistan. Lakini mtu huyu aliyebebeshwa lawama za matukio kadhaa ya kigaidi, alikuwa nani hasa?

https://p.dw.com/p/117ky
Osama bin Laden wakati wa uhai wake
Osama bin Laden wakati wa uhai wakePicha: AP

Kila mtu alikuwa akimjua, lakini hakuna aliyewahi kukutana naye. "Gaidi hatari kabisa wa dunia", kama Wamarekani walivyokuwa wakimwita, ameacha picha ya aina pekee: kilemba, mtu mwembamba, uso mweusi na macho malegevu na madevu. Sauti yake pia ilikuwa maarufu kutokana na kanda kadhaa za video na risala nyengine alizokuwa akitoa dhidi ya wanasasa wa Magharibi.

"Katika wakati ambapo madege yenu, vifaru vyenu vinabomoa nyumba wanamoishi watu wetu na watoto wetu huko Palestina, Iraq, Afghanistan, Chechniya na Pakistan, mnatucheka na kusema: 'Hatuihujumu dini ya Kiislam, hasha! Tunawahujumu magaidi na tunataka tuishi pamoja kwa amani, tuwe na majadiliano badala ya mapambano ya utamaduni.' Ukweli lakini unaonyesha mnasema uwongo. Wanasiasa wa Magharibi wanajidai wanataka majadiliano, wanatuhadaa ili kuvuta wakati: hawataki silaha ziwekwe chini, wanataka tusalimu amri." Aliwahi kusema kiongozi huyu wa Al-Qaeda.

Osama bin Laden alikuwa na mtazamo mkakamavu wa mema na maovu, wa haki na yasiyo ya haki. Na alikuwa na mali na ufasaha wa kuweza kuwashawishi watu.

Mtoto huyo wa kiume wa mmojawapo wa matajiri wakubwa wa Saudi Arabia, alianza kusimamia shughuli za kampuni yao tangu alipokuwa na umri wa miaka 15. Sambamba na hayo alikuwa akisomea ujenzi wa nyumba za ghorofa.

Mwaka 1982 Bin Laden, alipelekwa Afghanistan na idara ya upelelezi ya Saudi Arabia, wakati ule ilikuwa imevamiwa na vikosi vya Usovieti, ili akasimamie ujenzi wa mahandaki na ngome kwa ajili ya wanamgambo wa Mujahiddin. Aligharimia ujenzi wa kambi kadhaa za mafunzo kwa ajili ya wapiganaji wanaojitolea kutoka ulimwengu wa Kiislam.

Aliporejea Saudi Arabia mapema miaka ya '90, alilaani hadharani kuwepo wanajeshi wa Marekani nchini mwake na kutaka paundwe taifa la Kiislam. Alifukuzwa na kupokonywa uraia wake lakini sehemu ya milki ya kampuni ya ujenzi ya baba yake akaondoka nayo.

Akiishi kwanza nchini Sudan, lakini Marekani ilipoingilia kati kutaka afukuzwe, akarejea Afghanistan. Huko ndiko alikounda mtandao wa Al Qaida, kwa Kiswahili 'Shina', pamoja na Ayman Al Zawahiri, daktari wa kutoka Misri. Al Qaida wakaandaa mashambulio nchini Yemen, Somalia, Tanzania, Kenya, Saudi Arabia na mwishowe nchini Marekani.

Katika kanda ya video iliyotolewa baadaye, Bin Laden alikuwa akitafuta aungwe mkono katika mashambulio ya kikatili kabisa kuwahi kushuhudiwa: kuangamizwa majengo ya World Trade Center mjini New York na katika wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, Septemba 11 mwaka 2001. Mashambulio hayo yaligharimu maisha ya watu kadiri ya 3,000.

Mashambulio hayo ndio chanzo cha kuanzishwa mapambano dhidi ya ugaidi, miezi mitatu baadaye. Ushirika uliokuwa ukiongozwa na Marekani na kuhalalishwa na Umoja wa Mataifa ukaung'owa madarakani utawala wa Wataliban nchini Afghanistan.

Mwandishi: Saoub Esther (SWR)/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Josephat Charo