1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN:Amri ya Israel itawatesa raia Gaza

Angela Mdungu
11 Julai 2024

Umoja wa Mataifa umesema kuwa, amri ya jeshi la Israel ya kuwataka raia waondoke katika mji wa Gaza, utawasababisha wakaazi hao mateso makubwa

https://p.dw.com/p/4i9iy
Mashambulizi ya Israel Ukanda wa Gaza
Wakaazi katika Ukanda wa Gaza wakitazama uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Jeshi la IsraelPicha: EYAD BABA/AFP via Getty Images

Amri hiyo inatafsiriwa na waangalizi wa mzozo huo kuwa ishara ya operesheni mpya za kijeshi za Israel katika Ukanda wa huo. Ofisi ya kuratibu masuala ya kiutu ya Umoja wa Mataifa OCHA imetoa onyo hilo katika taarifa iliyoitoa Jumatano ikisema kuwa maelekezo yaliyotolewa na Israel ya kuwataka watu waondoke mjini Gaza yatachochea madhila makubwa kwa familia za Kipalestina ambazo zimekuwa zikilazimika kuhama hama mara nyingi kutokana na vita.

Soma zaidi: Israel yazidisha mashambulizi dhidi ya Gaza

Jeshi la Israel lilitoa amri hiyo kwa kudondosha maelfu ya vipeperushi kwenye mji wa Gaza ambao kulingana na Ofisi ya kuratibu masuala ya kiutu ya Umoja wa Mataifa unakaliwa na wakaazi 350,000.

Akizungumzia hatua hiyo ya Israel msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephen Dujarric amebainisha kwamba raia wanapaswa kulindwa na kupatiwa mahitaji yao bila kujali kuwa wanakimbia maeneo yao au la.

Pande hasimu zatakiwa kuheshimu utu

Dujarric pia alifafanua kuhusu njia ambazo wakaazi walioathiriwa na amri hiyo wanaweza kupita bila kukaguliwa na kuongeza kuwa Mji wa Gaza ni eneo hatari.  Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa, pia ametoa wito kwa pande zote zinazohusika kwenye mzozo kuheshimu sheria ya kimataifa kuhusu masuala ya kiutu.

Soma zaidi:UN yapinga wapalestina kuhamishwa Gaza 

Wakati huo huo  jeshi la Israel lilisema jana Jumatano kuwa, limekamilisha shughuli kwenye eneo la Shujaiya, mashariki mwa Gaza. Eneo hilo limekuwa uwanja wa mapambano kwa muda wa wiki mbili. Kulingana na taarifa ya jeshi hilo, lilifanikiwa kuyaharibu mahandaki mawili na kuwauwa magaidi kadhaa.

Jeshi la Israel lilianzisha mashambulizi mwanzoni mwa mwezi Mei katika eneo la wa Rafah linalopakana na Misri likilitaja kuwa ni ngome kubwa ya kundi la Hamas. Hata hivyo tangu hapo, mapigano yameongezeka kati ya wanajeshi hao na wapiganaji wa Kipalestina kaskazini na katikati mwa Ukanda wa Gaza.