1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel lakubali kusitisha mapigano kwa muda Gaza

16 Juni 2024

Jeshi la Israel limetangaza kusitisha mapigano kwa muda ili kuruhusu misaada kuingia kusini Mwa Gaza na kuwafikia Wapalestina wanaopitia hali mbaya ya kibinaadamu iliyosababishwa na vita kati ya Israel na kundi la Hamas

https://p.dw.com/p/4h6Ww

Vita hivyo vimeingia mwezi wake wa tisa tangu vilipoanza Oktoba 7 mwaka uliyopita. 

Kusitishwa kwa mapigano hayo kunakofanyika katika sehemu ndogo tu iliyo kilomita 12 kuelekea mji wa kusini wa Rafah, kumeshindwa kutimiza malengo ya Jumuiya ya Kimataifa na mshirika mkuu wa Israel, Marekani wanaotaka mapigano kusitishwa kikamilifu. 

UN yaishtumu Israel kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, Hamas kwa uhalifu wa kivita

Kulingana na Jeshi la Israel usitishwaji wa mapigano ulioanza saa mbili asubuhi utamalizika saa moja jioni. Hatua hiyo itafanyika kila siku hadi taarifa nyengine itakapotolewa. 

Iwapo mapigano hayo yatasitishwa yatatoa nafasi pana zaidi ya kushughulikia mahitaji makubwa ya Wapalestina ambayo yamezidi kutanuka hasa baada ya Israel kuanzisha  uvamizi wake mjini Rafah.