1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSaudi Arabia

OPEC+ yapunguza uzalishaji wa mafuta

5 Juni 2023

Saudi Arabia itapunguza uzalishaji wa mafuta baada ya mkutano wa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi ulimwenguni, OPEC ikiwa ni sehemu ya jaribio la kuongeza bei ya bidhaa hiyo licha ya hofu ya kudorora kwa uchumi.

https://p.dw.com/p/4SCWs
Muungano wa mashirika yanayozalisha mafuta kwa wingi zaidi ulimwenguni OPEC yamepunguza tena kiwango cha kuzalisha na kuzua hofu.
Ongezeko la bei ya mafuta limekuwa likizigusa sekta nyingi ulimwenguni, hatua inayosababisha bei za bidhaa nyingine kupanda.Picha: ALEXANDER KLEIN/AFP/Getty Images

Mataifa hayo yalikutana jana huko makao makuu ya OPEC, Vienna, Austria katika majadiliano yaliyoripotiwa kuwa magumu na yaliyoibuka na matokeo ambayo hayakutarajiwa. 

Hatua hii ya Saudi Arabia inahusisha kupunguza mapipa milioni moja na waziri wa nishati wa nchi hiyo, Prince Abdulaziz bin Salman aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano huo kwamba punguzo hilo la mwezi Julai linaweza kuongezwa. OPEC ina wanachama 13 wanaoongozwa na Saudi Arabia na washirika wake 10, wakiongozwa na Urusi.

Hatua hii ni tofauti na matarajio ya wachambuzi kwenye sekta hiyo, ambao kwa kiasi kikubwa walidhani wazalishaji hao wakubwa wataendeleza sera ya sasa. Lakini Saudi Arabia kwa mfano, inataka kuongeza bei ili kusawazisha bajeti yake.

Saudi Arabien | Öl-Lager am Hafen von Jubail
Picha: Bilal Qablan/AFP/Getty Images

Soma Zaidi: OPEC+ yaidhinisha hatua ya kupunguza uzalishaji wa mafuta

Wazalishaji wa mafuta kwa sasa wanakabiliana na si tu anguko la bei, bali pia kuyumba kwa soko katikati ya vita vya Urusi na Ukraine, ambavyo vimeathiri uchumi wa ulimwengu. Bei ya mafuta imeshuka kwa takriban asilimia 10 tangu baadhi ya mataifa yalipotangaza mwezi Aprili kupunguza bei kwa hiyari, huku mafuta ghafi yanayouzwa zaidi ulimwenguni ya Brent yakishuka kwa karibu dola 70 kwa pipa, kiwango ambacho hakijashuhudiwa tangu Desemba 2021.

Soma Zaidi: OPEC yapunguza ugavi huku kukiwa na hofu ya mfumuko wa bei

Wafanyabiashara wanahofia kwamba mahitaji yatapungua, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu hali ya uchumi wa dunia wakati Marekani ikipambana na mfumuko wa bei na viwango vya juu vya riba huku China ikionyesha kuwa katika mkwamo wa baada ya Covid-19.

Picha inayoonyesha mapipa ya kuhifadhia mafuta nchini Urusi
Urusi imesema itapunguza uzalishaji wa mafuta kwa mapipa 500,000 kwa mwezi ikiungana na mataifa makubwa ya uzalishaji wa mafuta ulimwenguni.Picha: Igor Onuchin/imago images/ITAR-TASS

Naibu waziri mkuu wa Urusi Alexander Novak amesema baada ya mkutano huo kwamba punguzo hili litakwenda hadi mwishoni wa mwaka 2024 baada ya suala hilo kufanyiwa uchunguzi wa muda mrefu.

"Makubaliano hayo yatakwenda hadi mwishoni mwa mwaka 2023. Leo tumejadili kwa muda mrefu uwezekano wa kurefusha hadi mwisho wa 2024. Kulikuwa na maamuzi mawili muhimu yaliyofanywa: Kwanza, kuongeza mkataba hadi mwisho wa 2024 na pili, ni juu ya upunguzaji huo wa hiari uliofanywa na nchi tisa kuanzia Mei Mosi wa mapipa milioni 1,660 kwa siku, utakaoenda hadi mwishoni mwa 2024. Hii itatupa fursa katika mtazamo wa muda mrefu kuwa na tathmini inayotabirika ya makubaliano yetu.," Novak aliwaambia waandishi wa habari.

Urusi ambayo pia inalenga kuendeleza punguzo la hiyari la uzalishaji wa mafuta iliufuatilia kwa karibu mkutano huo, na baada ya mkutano Novak alisema wao pia watapunguza mapipa 500,000 kwa siku hadi mwishoni mwa mwezi Disemba. Amesema hatua hiyo ni kama ya tahadhari tu na itaratibiwa na nchi zilizoshiriki katika makubaliano ya OPEC+, yaliyoanza mwezi Aprili.

Mchambuzi kutoka benki ya kimataifa ya UBS yenye makao yake, Uswisi Giovanni Staunovo amesema "kwa mara nyingine muungano huu umeonyesha mshikamano wao, kwa kuwa mwisho wa siku huwa ni juu ya kile wanachokubaliana, na hili ndilo la muhimu kwao."

Urusi inategemea mapato yatokanayo na mafuta, na hasa wakati huu inapopambana na Ukraine pamoja na vikwazo vya magharibi vilivyoathiri uchumi wake. Imekuwa ikiiuzia mafuta India na China.

Mataifa ya OPEC huzalisha karibu asilimia 60 ya mafuta kote ulimwenguni na mkutano mwingine wa ushirikiano huo umepangwa kufanyika Novemba 26.