1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na mkewe wampigia upatu Kamala Harris kuwa rais

21 Agosti 2024

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama na mkewe Michelle wamehutubia mkutano mkuu wa chama cha Democratic usiku wa kuamkia leo na kumpigia debe Kamala Harris kuwa mwanasiasa anayetosha kuiongoza nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4jjNI
Marekani | Obama na mkewe Michelle
Barack Obama na mkewe Michelle wakati wa mkutano mkuu wa Democratic. Picha: Alyssa Pointer/REUTERS

Katika hotuba zao zilizofuatiana Obama na mkewe, wameisifu rikodi ya kisiasa na utumishi ya Kamala Harris wakimwelezea kuwa kiongozi aliye tayari kubeba majukumu mazito ya kuingoza dola hiyo kubwa na yenye nguvu duniani.

Wote wawili wamesema tajriba ya Kamala Harris inatosha kuwasaidia Wamarekani kurejesha matumaini na kuipigania demokrasia dhidi ya Donald Trump ambaye wamekumbusha muhula wake wa miaka minne madarakani uligubikwa na tabia za "ujuba, kiburi na vurumai".

Ilikuwa ni Michelle Obama aliyefungua pazia la hotuba za wawili hao katika siku ya pili ya mkutano wa Democratic unaofanyika kwenye mji wa Chicago.

Yeye alitoa mwito kwa Wamarekani kupiga kura kwa wingi uchaguzi wa Novemba akisema wingi wa kura ndiyo utamudu kuwashinda wapinzani wao wa Republican.

Amesema anampigia upatu Kamala Harris kwa sababu historia ya maisha yake inafanana na ile ya Wamarekani wengi. Amesema Kamala amelelewa ndani ya familia ya kipato cha wastani, akafanya juhudi kupanda ngazi baada ya ngazi kufikia nafasi ya kuwa makamu wa rais wa nchi na kwa hivyo anazifahamu shida za walio wengi nchini humo.

Michelle hakusita kumtaja wazi wazi Donald Trump akikumbusha tabia yake kuwashambulia wengine kwa kejeli na maneno ya kutweza utu na amewaambia wapigakura wanaweza kumkataa kwa mara nyingine kwenye sanduku la kura.

"Hatma yetu iko mikononi mwetu. Ndani ya siku 77 zijazo, tunayo nguvu ya kuiepusha nchi yetu na vitisho na migawanyiko ya miaka iliyopita. Tunayo nguvu ya kubadili matumaini yetu kuwa vitendo. Tunayo nguyu ya kuulipa upendo, jasho na sadaka ya mabibi na mababu zetu waliokuwepo kabla yetu. Tumewahi kufanya hivyo na kwa hakika tunaweza kufanya hivyo kwa mara nyingine."

Obama asema wapiga kura wanaweza kuzuia miaka mingine minne ya Donald Trump 

Marekani, Chicago | Mkutano wa Democratic | Barack Obama
Barack Obama akihutubia mkutano mkuu wa Democratic. Picha: Eva Hambach/AFP/Getty Images

Kwa upande wake Obama alipokaribishwa na mkewe jukwaani alitumia maneno karibu sawa na ya Michelle akisema "Marekani iko tayari kwa mwanzo mpya" na kuwahimiza wapiga kura wasifanye makosa katika uchaguzi wa Novemba.

Obama ambaye ni moja ya Wademocrat mashuhuri nchini Marekani amewatahadharisha Wamarekani dhidi ya muhula mwingine wa Donald Trump

Mbali ya Obama na mkewe, mume wa Kamala Harris Doug Emhoff naye pia alihutubia mkutano wa Democratic na kumwelezea mkewe kuwa mtu mchangamfu na mpambanaji.

Mbali ya hotuba za watu mashuhuri usiku wa jana ulitumiwa pia na wajumbe wa Democratic kupiga kura ya wazi kumuuidhinisha Kamala Harris kuwa mgombea rasmi wa chama hicho.

Kura kama hiyo ilikwishapigwa kwa njia ya mtandao wiki kadhaa zilizopita lakini kwa desturi ilikuwa lazima wajumbe wasema hadharani kuwa kwa wingi wanamuunga mkono.

Wakati yote hayo yakiendelea ukumbini polisi ilipambana na waandamanaji wanaounga mkono Wapalestina na baadhi wametiwa nguvuni.

Maandamano yao yalianzia kwenye ubalozi mdogo wa Israel mjini Chiacago na kusambaa karibu na ukumbi wa mikutano. Waandamanaji wanataka vita visitishwe ukanda wa Gaza na mzozo huo unazingatiwa kuwa kihunzi kirefu kwa chama cha  Democratic katika uchaguzi wa Novemba.