1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama awataka Waislamu kupambana na al-Qaeda

Sekione Kitojo10 Novemba 2010

Obama ameisifu Indonesia kuwa ni mfano wa kuvumiliana kati ya mataifa ya Kiislamu na yale ya magharibi.

https://p.dw.com/p/Q3i8
Rais Barack Obama akihutubia katika chuo kikuu cha mjini Jakarta.Picha: AP

Rais Barack Obama jana Jumatano ameadhimisha mapinduzi yaliyofanyika nchini Indonesia kutoka utawala wa "mkono wa chuma", hadi katika utawala wa kidemokrasia na kuimwagia sifa tele nchi hiyo ambayo alikulia akiwa kijana kutokana na imani yao katika kuvumiliana na kusema kuwa ni mfano kwa Uislamu na mataifa ya magharibi.

Obama amesema kuwa mabadiliko ya Indonesia yameakisi katika maisha yake, miaka 40 tangu alipoondoka nchini humo, nchi ambayo ina idadi kubwa ya Waislamu duniani, akiwa kijana mdogo, akiwa njiani kuelekea kuwa rais wa Marekani.

Indonesia ni sehemu ya maisha yangu, Obama amesema, akimkumbuka marehemu mama yake akiwa ameolewa na mtu wa kutoka Indonesia na kwenda huko na mtoto wake huyo wa kiume mjini Jakarta , ambako alikuwa akirusha vishada, akicheza katika mashamba ya mpunga na kukamata wadudu.

Rais huyo wa Marekani alionyesha uwezo wake wa lugha ya Kiindonesia katika ziara yake hiyo ya saa 19 nchini humo, na kushangiliwa sana.

Katika hotuba yake aliyoitoa katika chuo kikuu mjini Jakarta, rais Obama amewataka Waislamu duniani kufanya kazi kwa pamoja na Marekani kupambana na kundi la kigaidi la al-Qaeda. Obama amerudia matamshi yake aliyoyatoa mjini Cairo mwaka jana kuwa Marekani haiko vitani na Uislamu, na kuzitaka pande zote mbili kutoangalia kwa jicho la shaka na kutoaminiani.

Sisi sote tunapaswa kuwashinda al-Qaeda na washirika wake, kwa kuwa hawana haki ya kujidai ni viongozi wa dini, na hasa sio dini kuu kama Uislamu, Obama amesema katika hotuba yake.

Wale wanaotaka kujenga, hawapaswi kuwapa nafasi magaidi ambao wanataka kuharibu, amesema. Hili si jukumu la Marekani pekee.

Obama amekiri kuwa kazi kubwa bado inapaswa kufanyika kuweza kuyaangalia masuala ambayo yamezusha mvutano baina ya Waislamu na Marekani , ikiwa ni pamoja na mzozo wa Mashariki ya Kati pamoja na vita vinavyoongozwa na Marekani nchini Iraq na Afghanistan.

Tunaweza kuchagua kujibainisha kutokana na tofauti zetu, na kutumbukia katika hali ya shaka na kutoaminiana. Ama tunaweza kuchagua kazi ngumu ya kujaribu kupata maelewano na kutafuta njia za maendeleo. Na naweza kuwaahidi kuwa ,licha ya vikwazo vinavyoweza kutokea, Marekani inataka maendeleo ya binadamu.

Obama ameisifu Indonesia kwa hatua ilizopiga katika kuwaondoa magaidi pamoja na kupambana na watu wenye imani kali ya kidini.

Indonesia imewauwa na kuwaweka kizuizini wapiganaji kadha wa Kiislamu ambao walihusika katika mashambulizi kadha nchini humo katika miaka ya hivi karibuni, hususan shambulio la bomu katika mji wa kitalii wa Bali, ambapo watu 202 waliuwawa.

Mapema jana , Obama alitembelea msikiti mkubwa kabisa nchini Indonesia , msikiti wa Istiqlal, akionyesha mshikamano na Waislamu. Katika ziara hiyo, akiwa pamoja na mkewe, Michelle , aliongozwa na imam wa msikiti huo Haji Mustapha Ali Yaqub.

BdT Ramadan in Indonesien
Waumini wakiswali katika Msikiti mkubwa kabisa nchini Indonesia wa Istiglal ,ambao rais Obama na mkewe waliutembelea.Picha: AP

Msikiti huo uko karibu na kanisa kuu la mjini Jakarta, na wakati wa Chrismas , viongozi wa msikiti huruhusu waumini wa Kikristo kutumia eneo la msikiti la kuegesha magari , kwasababu wao hawana nafasi kubwa. Huo ni mfano wa ushirikiano baina ya dini nchini Indonesia, Obama amesema.

Obama ameondoka nchini Indonesia saa mbili kabla ya kumalizika kwa ziara yake kutokana na moshi unaotoka katika mlima wa volkano, akiwa njiani kuelekea Korea ya kusini ambako atahudhuria mkutano wa kundi la mataifa ya G20 unaoanza kesho Alhamis.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe/dpae

Mhariri: Miraji Othman