1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama asifu msimamo mmoja dhidi ya Urusi

Admin.WagnerD26 Machi 2014

Rais wa Marekani Barack Obama amesifu ushirikiano baina ya nchi yake na nchi za Ulaya katika kukabiliana na changamoto za kimataifa, ikiwemo namna zilivyozishughulikia hatua za Urusi katika mgogoro wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/1BW98
Rais Obama, Herman Van Rampuy na Jose Manuel Barroso katika mkutano na waandishi
Rais Obama, Herman Van Rampuy na Jose Manuel Barroso katika mkutano na waandishiPicha: Reuters

Hayo Rais Obama ameyasema katika hotuba yake mjini Brussels muda mfupi uliopita, baada ya mkutano kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya. Mkutano huo uligubikwa na masuala mawili muhimu, ambayo ni makubaliano ya kibiashara yanayojadiliwa kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya, na mgogoro wa hivi karibuni unaoihusu Ukraine.

Akizungumza na waandishi wa habari sambamba na rais wa Umoja wa Ulaya Herman van Rompuy na rais wa halmashauri kuu ya Umoja huo Jose Manuel Barroso, Rais Obama amesema iwapo makubaliano hayo kibiashara kati ya Marekani na Ulaya yatasainiwa, yataweka uwezekano kwa Marekani kuiuzia Ulaya nishati ya gesi, na hivyo kupunguza hali ya sasa ya nchi za Ulaya kutegemea sana Urusi kwa nishati hiyo.

Hofu ya nchi dhaifu

Rais Obama ametuliza hofu ya nchi ambazo zinatilia mashaka tija itakayotokana na biashara huria itakayotokana na makubaliano, akizitaka kuwa na subira na kufuatilia kwa makini yaliyopo kwenye mazungumzo, kabla ya kutoa hukumu kwa makubaliano ambayo bado hayajapatikana.

Rais Barack Obama akizungumza mjini Brussels
Rais Barack Obama akizungumza mjini BrusselsPicha: Reuters

Na kuhusu mgogoro wa Ukraine ambao umekuwa afenda kubwa kwenye ziara ya rais Obama barani Ulaya, rais huyo wa Marekani amesema ikiwa Urusi ilidhani ingeweza kuutumia mgogoro huo kuweka pengo kati ya Ulaya na Marekani, basi mahesabu yake iliyafanya vibaya. Obama amesifu namna pande hizo, yaani Marekani na Umoja wa Ulaya zilivyoshirikiana dhidi ya Urusi katika mgogoro huo.

''Marekani na Umoja wa Ulaya zimekuwa na msimamo mmoja kuhusu suala hili. Tumezungumza kwa sauti moja kuiunga mkono Ukraine na kuelezea haja ya kuinga mkono na kuutuliza uchumi wake. Tumeungana kuhusu usalama wa Ulaya, na katika kuitenga Urusi na kuiadabisha kwa matendo yake.'' Amesema Obama.

Doa la udukuzi kwenye haiba ya Marekani

Mkutano huu kati ya Marekani na Ulaya umefanyika wakati kukiwa bado kuna doa kwenye haiba ya Marekani, kufuatia kufichuliwa kuwa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani lilikuwa likifanya udukuzi katika mawasiliano ya viongozi wa nchi washirika barani Ulaya, na viongozi wa Umoja wa Ulaya wamewasilisha malalamiko yao kwa rais Obama, wakitaka raia wa Marekani na wa Ulaya wapate haki sawa ya kutoingiliwa katika faragha yao.

Hatua ya Urusi kuiingiza Crimea kwenye himaya yake imekuwa agenda kubwa katika ziara ya Obama Ulaya
Hatua ya Urusi kuiingiza Crimea kwenye himaya yake imekuwa agenda kubwa katika ziara ya Obama UlayaPicha: Reuters

Rais Obama amesema atachukua hatua zinazofaa kuyashughulikia malalamiko hayo.

Aidha, Obama amesema Umoja wa kujihami wa NATO hauna budi kuwa karibu sana na nchi wanachama ambazo ni dhaifu kijeshi na ambazo zinahofia usalama wao kutokana na kuwa karibu na mpaka wa Urusi. Hata hivyo alipoulizwa kuhusu uwezekano wa nchi kama Ukraine na Georgia kuingizwa katika NATO, rais Obama amesema hakuna mpango wa haraka wa kuupanua umoja huo wa kujihami.

Hali kadhalika ameelezea wasi wasi kuhusu hatua ya baadhi ya nchi wanachama wa NATO kupunguza kwa kiasi kikubwa bajeti zao za kijeshi, na kuonya kwamba uhuru hauwezi kupatikana kwa bei rais.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/DPAE/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman