1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nusu ya vifo vya corona Ulaya ni vya kwenye nyumba za wazee

23 Aprili 2020

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema nusu ya vifo vilivyotokea barani Ulaya kutokana na virusi vya corona vilikuwa katika nyumba za kuwaangalia wazee.

https://p.dw.com/p/3bJtF
Deutschland Altenpflege Coronavirus
Picha: picture-alliance/dpa/J. Güttler

Katika mkutano na waandishi habari, Mkurugenzi wa WHO barani Ulaya, Dokta Hans Kluge, ameielezea picha inayotia wasiwasi kwenye nyumba za wazee kutokana na athari ya virusi vya corona, ambako huduma ya kuwatunza wazee mara nyingi imekuwa ikipuuzwa.

"Kulingana na makadirio kutoka kwenye nchi za Ulaya, hadi nusu ya watu waliokufa kwa ugonjwa wa COVID-19 walikuwa wakiishi kwa muda mrefu kwenye vituo vya kuwaangalia wazee. Hili ni janga la kibinaadamu ambalo haliwezi kufikirik," alifafanua Kluge.

Kluge amesema wafanyakazi wa afya katika taasisi hizo ambao mara nyingi wanazidiwa na kazi na kulipwa mshahara mdogo ni mashujaa wasiotajwa wa janga hili. Ametoa wito kwa wafanyakazi hao kupewa vifaa vya kujikinga pamoja na msaada zaidi.

Visa vyaongezeka Ulaya Mashariki

Kwa mujibu wa Kluge, licha ya dalili za utulivu, mzozo huo uko mbali sana kukamilika na kwamba visa vya wiki iliyopita viliongezeka katika eneo la mashariki mwa Ulaya, hasa kwenye nchi za Urusi, Uturuki, Ukraine, Uzbekistan na Belarus. Hivi sasa karibu nusu ya maambukizi ya dunia na vifo viko barani Ulaya.

Hayo yanajiri wakati ambapo viongozi wa Umoja wa Ulaya wanajaribu kuanzisha mpango wa kuufufua uchumi wa bara hilo ambao umekumbwa na changamoto kutokana na virusi vya corona. 

Coronavirus Russland Moskau Bürgermeister besucht Krankenhaus
Madktari katika hospitali ya Urusi inayowaangalia wagonjwa wa virusi vya coronaPicha: picture-alliance/AP/Mayor Press Service/D. Grishkin

Ajenda kuu ya mkutano huo unaofanyika leo kwa njia ya video ni kuhusu mfuko wa kuukarabati uchumi wa umoja huo wenye thamani ya matrilioni ya Euro kama jibu la kuporomoka kwa uchumi, ingawa kuna matumaini kidogo ya kupatikana suluhisho la haraka.

Kwa mujibu wa duru za Umoja wa Ulaya, tofauti kati ya nchi za umoja huo hasa katika suala la kusaidiana deni ili kuongeza fedha kwa ajili ya kuufufua uchumi, bado ni kubwa.

Hadi sasa kuna zaidi ya visa milioni 1.1 vya virusi vya corona barani Ulaya na zaidi ya vifo 110,000. Muongo mmoja baada ya mzozo wa madeni wa Ulaya, janga la COVID-19 linaamsha tena mizozo ya zamani na kuupima uwezo wa Umoja wa Ulaya katika kupata majibu yaliyoratibiwa.

Wakati huo huo, Afrika imerekodi ongezeko la asilimia 43 la maambukizi ya virusi vya corona katika kipindi cha wiki moja iliyopita, hali inayozusha hofu kuwa huenda bara hilo likawa linalofuatia kwa kuathiriwa zaidi.

Mkurugenzi wa kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa barani Afrika, CDC, John Nkengasong amesema bara hilo lenye watu bilioni 1.3 lina uwezo mdogo sana wa kuwapima watu, huku likiwa na vifaa vya upimaji ambavyo ni dhaifu.

Hivi karibuni WHO ilitoa ripoti inayoonya kuwa janga la COVID-19 linaweza kusababisha takriban vifo 300,000 barani Afrika, huku likiwaingiza watu milioni 30 katika umasikini.


(DPA, AFP, AP)