1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Niger yasitisha uchimbaji madini hadi ukaguzi ufanyike

25 Januari 2024

Serikali ya kijeshi nchini Niger imesimamisha kwa muda utoaji wa leseni mpya za uchimbaji wa madini na kuagiza ukaguzi wa sekta hiyo, kwa mujibu wa wizara ya madini nchini humo.

https://p.dw.com/p/4beXW
Urani Niger Orano
Mojawapo wa migodi ya kuchimba madini ya urani nchini Niger inayomilikiwa na kampuni ya Orano ya Ufaransa.Picha: Issouf Sanogo/AFP/picture alliance/dpa

Hata hivyo, wizara hiyo haikueleza sababu za kusitishwa kwa utoaji wa leseni katika taarifa yake ya Januari 22 iliyoonekana na shirika la habari la Reuters siku ya Alkhamis (Januri 25).

Waziri wa madhini pia hakutaka kuzungumzia hatua hiyo alipoombwa na shirika hilo.

Taifa hilo la magharibi mwa Afrika lina hifadhi kubwa ya madini ya kiwango cha juu ya urani na ni la saba ulimwenguni kwa kuwa na madini hayo, yanayotumika pia katika utengezaji wa nishati ya nyuklia.

Niger ina kiwanda kikubwa cha usanifishaji urani kinachoendeshwa na kampuni ya Ufaransa ya Orano, ambacho kimeendeleza shughuli zake licha ya mapinduzi ya Julai mwaka uliopita.