Niger yajiandaa na maandamano makubwa ya kuipinga Ufaransa
1 Septemba 2023Muungano wa makundi ya asasi za kiraia yanayopinga uwepo wa vikosi vya Ufaransa nchini humo, umeitisha maandamano ya siku tatu kuanzia leo Ijumaa.
Maandamano hayo yaliyoandaliwa na kundi la M62, yatafanyika katikati mwa mji mkuu wa Niamey yakishinikiza kuondoka kwa maafisa wa Ufaransa. Ufaransa inao askari wapatao 1,500 nchini humo wengi wakiwa katika kambi ya anga karibu na mji mkuu ambao walikuwa wakisaidia kupambana na wanamgambo.
Hayo yakijiri, Umoja wa Mataifa umesema leo kuwa unatafuta mawasiliano na viongozi wa mapinduzi wa Niger , baada ya wanajeshi hao kusimamisha shughuli za mashirika na taasisi zake nyingine kufanya kazi katika maeneo ya operesheni za kijeshi.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Alessandra Vellucci mjini Geneva, amesema kuwa wameziona ripoti hizo na kwa hivi sasa wanatafuta kuwasiliana na mamlaka za kijeshi nchini Niger, kupata ufahamu zaidi na athari zake kwa kazi za kiutu.