1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni mwaka mmoja baada ya shambulizi la mjini Berlin

Isaac Gamba
19 Desemba 2017

Ujerumani  hii leo inakumbuka mwaka moja kamili tangu kufanyika kwa shambulizi la lori  lililosababisha vifo vya watu 12 na kujeruhi wengine 70 katika soko la Krismasi mjini Berlin.

https://p.dw.com/p/2pcP2
Deutschland Angela Merkel besucht Breitscheidplatz nach Terroranschlag NEU
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Sohn

Soko hilo maarufu la Krismasi lililoko katika eneo la Breitscheidpaltz mjini Berlin litafungwa hii leo kwa siku nzima ikiwa ni ishara ya heshima kwa wahanga wa shambulizi hilo lililofanywa na raia wa Tunisia ambaye maombi yake ya kupatiwa hifadhi nchini Ujerumani yaligonga mwamba.

Kumbukumbu hizo za mwaka mmoja za shambulizi  zinafanyika  siku moja baada ya  Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kukutana na ndugu wa wahanga  wa tukio hilo kwa mara ya kwanza ikiwa ni baada ya kukosolewa kwa kushindwa kukutana nao mapema.

Rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeir anatarajiwa kutoa hotuba kwenye kumbukumbu hiyo itakayofanyika katika  kanisa lililopo  eneo hilo  itakayofuatiwa na uzinduzi wa mnara wa kumbukumbu wenye urefu wa mita 14 uliyopakwa rangi ya dhahabu na uliyoandikwa majina ya wahanga wa tukio hilo.

Jioni ya leo watu watapata nafasi kushiriki maombi hayo katika muda ule ule ambao Anis Amri aliendesha lori katika soko hilo la Krismasi lililokuwa limefurika watu ambapo pia kengele za kanisa zitalia kwa dakika 12.

Tunesien Bruder hält Portrait von Anis Amri
Raia wa Tunisia Anis Amri aliyetekeleza shambulizi la lori mjini BerlinPicha: Getty Images/AFP/F. Belaid

Amri aliuawa kwa kupigwa risasi siku nne baada ya shambulizi hilo na polisi nchini Italia ambako aliwahi kuishi.

Kurt Beck  afisa aliyepewa jukumu na serikali ya Ujerumani kufuatilia na kushughulikia madhara yaliyotokana na shambulizi hilo amekiri hapo jana Jumatatu kuwa Kansela  Merkel alichelewa kukutana na familia za wahanga wa shambulizi hilo la mwaka jana.

Serikali yakiri mapungufu yaliyojitokeza baada ya shambulizi

Kanzlerin Angela Merkel CDU
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com/O. Messinger

Naye Kansela Merkel akizungumzia lawama hizo dhidi yake alikiri na kusema   ni wazi kwamba machungu waliyo nayo ndugu wa wahanga wa shambulizi hilo la mwaka jana hayawezi kupoozwa kirahisi lakini hata hivyo watafanya kila watakaloweza kuboresha masuala yanayostahili  kuboreshwa.

 Jeshi la polisi nchini Ujerumani nalo pia limekosolewa baada ya kubainika kuwa  Anis Amri aliyewasili nchini Ujerumani  wakati wa majira ya kiangazi  mwaka 2015 na kujisajili kwa utambulisho tofauti tofauti alipaswa kuwa amefukuzwa kabla ya kutekeleza shambulizi hilo.

Jumapili iliyopita gazeti la Welt am Sonntag nchini Ujerumani liliripoti kuwa Anis Amri alikuwa akifuatiliwa nyendo zake kwa karibu na majasusi wa Ujerumani tofauti na ilivyofikiriwa awali.

Waziri wa sheria wa Ujerumani Heiko Maas naye pia amesema serikali ya Ujerumani haikuwa imejiandaa kiasi cha kutosha kwa athari zitakazowakumba wahanga wa mashambulizi ya aina hiyo na kuongeza kuwa kutokana na mapungufu hayo serikali inachopaswa kufanya ni kuomba radhi.

Maas amependekeza kuanzishwa  idara ya uratibu serikalini kwa ajili ya  kushughulikia majanga kama hayo ili muhanga yeyote wa mashambulizi yanayoweza kutokea siku zijazo apate mara moja mtu wa kushughulikia masuala yake katika ngazi ya kiserikali.  Aidha ametoa mwito wa sheria kufanyiwa marekebisho ili  wahanga wote wa mashambulizi ya kigaidi wahudumiwe na kulipwa fidia sawa sawa bila kujali utaifa wao au silaha zilizotumika katika shambulizi.

 Wakati huohuo watu wamekuwa bado wakiendelea kumiminika katika soko hilo la Krismasi ingawa kumbukumbu ya shambulizi hilo la mwaka jana bado zina gonga katika mioyo.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE/DW

Mhariri: Iddi Ssessanga