1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New Zealand kuimarisha sheria ya umiliki wa bunduki

Daniel Gakuba
18 Machi 2019

Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern amesema mnamo siku chache zijazo atatangaza sheria mpya kuhusu umiliki wa bunduki katika nchi hiyo, baada ya shambulizi kwenye misikiti miwili ambamo watu 50 waliuawa.

https://p.dw.com/p/3FE6Y
Neuseeland PK Jacinda Ardern
Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda ArdernPicha: Getty Images/H. Hopkins

Katika mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na shambulizi la kigaidi la wiki iliyopita, Waziri Mkuu Jacinda Ardern amesema katika muda wa siku 10 atakuwa ametangaza mabadiliko katika sheria ya umilikaji wa bunduki, ambayo amesema anatumai itaifanya hali nchini  New Zealand kuwa salama zaidi. Mkutano huo umefuatia kikao cha baraza la mawaziri kilichoongozwa na Bi Ardern, ambapo mawaziri wote wamekubaliana kimsingi kuhusu mageuzi hayo.

Shambulizi la mtu mwenye itikadi kali ya mrengo wa kulia dhidi ya misikiti miwili Ijumaa iliyopita katika mji wa Christchurch liliuwa watu 50 na kuwajeruhi wengine wengi.

Mtazamo kuhusu bunduki wabadilika milele

Katika mkutano huo na waandishi wa habari waziri mkuu Jacinda Ardern alikuwa pamoja na naibu wake Winston Peters, kiongozi wa chama cha New Zealand First ambacho ni mshirika katika serikali. Siku za nyuma chama hicho kilipinga mabadiliko katika sheria ya bunduki, lakini wakati huu kimebadilisha mawazo.

Neuseeland Terroranschlag auf Moscheen in Christchurch | Polizeipräsenz
Ulinzi umeimarishwa mjini ChristchurchPicha: Reuters/E. Su

Kiongozi wake, Winston Peters amesema shambulizi la Ijumaa iliyopita limebadilisha hali ya mambo milele, na kwa hivyo sheria pia zinapaswa kubadilika. Sheria za New Zealand kuhusu umilikaji binafsi wa bunduki zilikuwa legevu sana, na waziri mkuu Ardern amesema raia wengi wamekuwa wakiitilia shaka.

''Nimeeleza bayana kwamba wa-New Zealand wengi wamekuwa wakiuliza maswali kuhusu upatikanaji wa silaha za kivita mikononi mwa watu nchini. Hata hivyo, jibu kamili nitalitoa baada ya kuyashughulikia maamuzi ya baraza la mawaziri la leo. Bado yapo mambo ya msingi yanayopaswa kutazamwa kwa kina, nataka kufanya hivyo, haraka iwezekanavyo." Amesema Ardern.

Makampuni ya mitandao ya kijamii yaingia matatani

Neuseeland Terroranschlag auf Moscheen in Christchurch | Trauer
Umma wa New Zealand umeungana kulaani shambulizi hilo la kigaidiPicha: picture-alliance/dpa/Matrixpictures

Suala jingine aliloliangazia Waziri Mkuu Ardern ni la makampuni ya mitandao ya kijamii, ambayo yaliruhusu muuaji kurusha moja kwa moja uovu aliokuwa kiufanya kwenye mtandao wa facebook. Kijana mbaye jina lake halikutajwa pia amekamatwa na kufikishwa mahakamani leo, kwa shutuma za kusambaza mitandaoni vidio ya mauaji hayo.

Taarifa zaidi zimeeleza kuwa mshukiwa wa mauaji hayo ya kigaidi Brenton Tarrant ambaye anajinadi kama mfuasi sugu wa itikadi zinazowaona Wazungu kuwa bora kuliko watu wengine, amemfukuza wakili wake, akiamua kujisimamia mwenyewe mahakamani.

Wakati huo huo familia zilizowapoteza watu wao katika shambulio la miskitini la Ijumaa iliyopita wanaendelea kuomboleza, wakifarijiwa na umma wa New Zealand katika ngazi zote. Hata hivyo bado wanasubiri miili ya wapendwa wao ili waweze kuizika kulingana na taratibu za Kiislamu, ambazo kwa kawaida zinahimiza Marehemu kuzika katika muda wa saa 24 baada ya kuaga dunia.

afpe, rtre