1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK : Zimbabwe yatakiwa kukomesha uhamishaji wa walala hoi

22 Julai 2005
https://p.dw.com/p/CEru

Ripoti muhimu ya Umoja wa Mataifa imeishutumu vikali serikali ya Zimbabwe kwa kuvunja nyumba za vitongoji duni zilioko mijini na kusisitiza kwamba serikali hiyo inapaswa kukomesha kuteketeza mitaa hiyo ya mabanda.

Hayo yamebainishwa na wajumbe wawili wa Umoja wa Mataifa ambao wameiona repoti hiyo ndefu inayotarajiwa kutolewa leo hii.

Repoti hiyo iliyoagizwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan inavunja ukimya ulioko Umoja wa Mataifa juu ya sera za Rais Robert Mugabe za kuwahamisha mamia na maelfu ya watu. Mataifa ya magharibi yalijaribu bila ya mafanikio kulifikisha suala hilo kwenye agenda ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Anna Tibaijuka wa Tanzania ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa shirika la Makaazi la Umoja wa Mataifa lenye makao yake mjini Nairobi Kenya ambaye ndie aliyeandika repoti hiyo amesema zaidi ya watu milioni mbili kwa njia moja au nyengíne wameathirika na bomowa bomowa hiyo ya makaazi ya vitongoji duni.