1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK : Wanajeshi 9 wa Umoja wa Mataifa wauwawa Congo

26 Februari 2005
https://p.dw.com/p/CFay

Umoja wa Mataifa umesema wanajeshi wake 9 wa kulinda amani kutoka Bangladesh wamevamiwa na kuuwawa na wengine 11 kujeruhiwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Wanajeshi wengine 4 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa ambao walikuwa hawajulikani walipo hivi sasa wamepatikana wakiwa salama.Doria ya walinda amani hao ilishambuliwa katika wilaya ya Ituri yenye utajiri wa madini ambapo kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Congo MONUC kina takriban wanajeshi 5,000 kutoka Pakistan,Bangladesh,Morroco na Nepal.

Kikosi hicho kimekuwa kikijaribu tokea mwezi wa Desemba kuyavunja makundi sita ya wanamgambo ambayo yamekuwa yakiwabughudhi wanakijiji.Hapo Alhamisi kikosi hicho cha MONUC kiliwakamata wanamgambo watuhumiwa 27 katika mji wa Datule.

Wafanya kazi wa misaada wamesema mapambano katika kipindi cha miezi miwili iliopita yamewapotezea makaazi raia 70,000.