1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Wanaharakati wawili wa kike wa haki za binaadamu watunukiwa Nobeli ya Afrika-

Jean-François M Gisimba14 Oktoba 2003
https://p.dw.com/p/CHeO

Maeza Ashenafi kutoka Ethiopia, na Sara Longwe kutoka Zambia, walitunukiwa tunzo ya kila mwaka ya bara la Afrika ya uongozi bora, ambayo mwaka huu ilikua inatolewa kwa mara ya kumi na tano kila mwaka. Tunzo hiyo inaelezewa kua ndiyo tunzo ya amani ya Nobel, kwa bara la Afrika.
Sherehe hio ilifanyika mjini New York , Marekani.

Tunzo hiyo, ina thamani ya kitita cha dola za Marekani elfu hamsini, ambazo hutolewa na taasisi ya kimataifa ya kupiga vita njaa, The Hunger Project.

Tunzo hiyo huzawadiwa wanaharakati na watetezi wa haki za binaadamu barani Afrika.

Maeza Ashenafi na Sara Longwe, ni watetezi wakubwa wa haki za binaadamu katika nchi zao Ethiopia na Zambia, lakini pia barani Afrika kote.

Maeza Ashenafi, ni muanzilishi na mwenyekiti wa chama cha wanasheria wa kike nchini Ethiopia. Chama hicho kimekua kikiendesha kampeni za kuendeleza elimu kwa wanawake wa nchi hio, na kuwatetea dhidi ya ukandamizaji wanaofanyiwa.

Miaka miwili iliyopita, serikali ya Ethiopia iliwahi kusitisha harakati za chama hicho, kutokana na malalamiko ya wanaharakati wa chama hicho, ya kutaka waziri wa sheria ajiuzulu, kutokana na kushindwa kwake kuadhibu watu wanaonyanyasa wanawake wanaofanya kazi za nyumbani, au wanaume wanaopiga wake zao.

Waliopendekeza jina la Maeza Ashenafi, wanasema mama huyo amefanya kazi ngumu ya kutetea haki za wanawake, katika nchi ambako hadi mwaka jana wa 2002, ni asilimia thelathini na sita ya wanawake pekee ndio walikua wanajua kusoma na kuandika, ambako asilimia ishirini na nane pekee ya watoto wa kike ndio walifanikiwa kuingia katika shule za msingi; katika nchi ambayo ina watu wasiopungua miliyoni mbili, walioambukizwa virusi vinavyosababisha ukimwi, wengi wao wakiwa ni wanawake, huku mila na tamaduni za baadhi ya makabila ya Ethiopia, zikiwa zinamuzuia mwanamke kujiendeleza kielimu, na kiuchumi.

Maeza Ashenafi amewaambia waandishi wa habari kwamba licha ya hali hio hajakata tamaa.

Akasema kumekuwepo maendeleo fulani, ingawa bado njia ni ndefu sana; akitoa mfano kwamba wakati akisomea sheria katika chuo kikuu, alikua msichana pekee darasani, lakini leo hii, wanawake ni takriban asilimia ishirini ya wanafunzi wote wa kitivo cha sheria katika chuo kikuu cha mji mkuu wa Ethiopia Addis Abbaba.

Bibi Sara Longwe, yeye amekua akiendesha kampeni zake za kuendeleza wanawake, katika maeneo ya vijijini nchini Zambia.

Kwa zaidi ya miaka sita, alikua mwenyekiti wa chama cha wanawake wa kiafrika, cha maendeleo na mawasiliano, kwa ufupi FEMNET.

Longwe ameliambia shirika la habari IPS, kwamba amejikuta hana lingine, ila tu kutetea wanawake wenzie, kwa sababu kamwe hawahusishwi katika kuchukua uamuzi, jambo ambalo linawafanya kusalia katika hali ya umasikini, na kutegemea wanaume.

Sara Longwe ameliambia shirika hilo la habari, kwamba licha ya pesa nyingi zinazopewa serikali ya nchi yake zambia, kuisaidia kupambana na ugonjwa hatari wa ukimwi, pesa hizo haziwafikii walengwa, ambao wengi wao ni wanawake.
Akasema wakati umewadia, ili serikali za nchi za magharibi na mashirika ya wafadhili, yawe yakizipatia serikali za nchi za bara la Afrika, masharti ya kuboresha huduma kwa jamii, hususan kwa wanyonge ambao wengi wao ni wanawake, ili kuzipatia serikali hizo misaada ya fedha.

Bibi Maeza Ashenafi na Mwenzie Sara Longwe, wametumia nafasi ya sherehe ya kuwakabidhi tunzo ya bara la Afrika ya Nobel, ili kusisitiza kwamba serikali za nchi za bara la Afrika lazima zipige vita ufisadi na rushwa, ziendeleze uongozi bora, na ndipo zitaweza kufikia viwango vya kuridhisha vya kuheshimu haki za binaadamu, hususan haki za wanyonge, ambapo barani Afrika, wengi wao ni wanawake.