1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK : Kanuni mpya kwa walinda amani wanaokiuka haki za binaadamu

24 Machi 2005
https://p.dw.com/p/CFU5

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaoshutumiwa kwa dhuluma za ngono pamoja na ukiukaji mwengine wa haki za binaadamu wanapaswa kushtakiwa katika mahkama za kijeshi katika nchi ambapo makosa hayo yametendeka .

Repoti kutoka kwa balozi wa Jordan kwenye Umoja wa Mataifa Prince Zeid la Hussein inatarajiwa kupendekeza hayo leo hii. Hussein ambaye aliwahi kutumika kama mwanajeshi wa kulinda amani huko Bosnia aliombwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan kuchunguza madai ya ukiukaji huo wa haki za binaadamu uliofanywa na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Congo pamoja na kupendekeza mabadiliko.

Akizungumza na mabalozi wa Ulaya Husssein amesema wanajeshi wa kulinda amani wanaoshutumiwa kwa dhuluma za ngono wasiachiliwe kurudi nyumbani kama ulivyo utaratibu wa hivi sasa hadi hapo watakapokuwa wamehukumiwa na mahkama za kijeshi katika nchi ambapo makosa hayo yametendeka.

Baada ya kuibuka kwa madai ya dhuluma na unyonnyaji wa kingono dhidi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo maafisa wa Umoja wa Mataifa wamekuwa na hofu kwamba ukiukaji huo wa haki za binaadamu yumkini ukawa ni tatizo katika nchi zote 17 duniani ambapo kuna vikosi hivyo vya Umoja wa Mataifa.

Madai kama hayo tayari yamezuka nchini Liberia na kwa kiasi fulani nchini Ivory Coast,Burundi na Haiti.